DPP awafutia mashitaka 10 ya utakatishaji fedha aliyekuwa bosi wa NIDA na wenzake wawili

NA MWANDISHI MAALUM

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) amewafutia mashitaka 10 ya utakatishaji fedha washtakiwa watatu kati ya watano akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu.
Mbali na Maimu washitakiwa wengine waliofutiwa mashitaka hayo ni aliyekuwa Ofisa Usafirishaji NIDA, George Ntalima na Xavery Silverius maarufu Silverius Kayombo waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Awali washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka 55 likiwemo utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya amedai leo Oktoba 22 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa, lakini wanakusudia kufanya mabadiliko katika hati ya mashtaka.

Amedai kesi hiyo ipo katika hatua za usikilizwaji, lakini Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) amekusudia kufanya marekebisho madogo chini ya kifungu cha 234(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

"Jumla ya mashtaka yaliyokuwa yanawakabili ni 55, baada ya marekebisho haya yatakuwa mashtaka 45, kwa mshtakiwa wa kwanza Dickson Maimu, mshtakiwa wa tatu, George Ntalima na wa nne Xavery Silverius maarufu Silverius Kayombo ambao wameondolewa mashtaka ya utakatishaji fedha," amedai Wakili Komanya.

Wakili Komanya amedai endapo hakutakuwa na pingamizi, wangeomba kuwasilisha hati mpya, hata hivyo hati hiyo haikupokelewa kutokana na Hakimu Mkazi Mkuu Rashid Chaungu anayesikiliza kesi kutokuwepo.

"Hata mkiwasilisha hati mpya, kesi hii haiko haiko mbele yangu, nawashauri muiwasilishe mbele ya Hakimu husika tarehe itakayopangwa, na kuhusu dhamana nawashauri kuwasilisha maombi Mahakama Kuu," alieleza Hakimu Shaidi.

Hata hivyo, baada ya maelezo hayo kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 4, mwaka itakapotajwa ambapo upande wa mashtaka utawasilisha hati mpya.

Katika kesi hiyo, tayari upande wa mashitaka umeshafunga ushahidi kwa kuwaita jumla ya mashahidi 26 pamoja na kuwasilisha vielelezo 45.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Meneja Biashara wa (NIDA), Aveln Momburi na Mkurugenzi wa Sheria, Sajina Raymond.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news