HOPE FOR GIRLS AND WOMEN IN TANZANIA WAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA KIKE KWA KUGAWA TAULO ZA KIKE, KUTOA ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA SHULENI

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya Ukatili wa Kijinsia mkoani Mara, limeadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike kwa kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia na kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu wanaosoma katika Shule ya Sekondari Buhemba na Mirwa zilizopo Wilaya ya Butiama.
Debora Boniphace ambaye ni Afisa Miradi kutoka Shirika la HGWT akizungumza na wanafunzi wa Mirwa Sekondari wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa kike.
Afisa Miradi kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT), Debora Boniphace amesema kuwa lengo la kugawa taulo katika shule hizo ni kuwawezesha wanafunzi wa kike kumudu kuhudhuria masomo yao, kwani baadhi yao hushindwa kuhudhuria shule wanapokuwa hedhi na kupelekea kukosa baadhi ya vipindi, huku elimu ya Ukatili wa Kijinsia akisema itawasaidia kutambua madhara na kuchukua hatua ikiwemo kuwaelimisha wengine na jamii.

Ameongeza kuwa, kwa kutambua umuhimu na thamani kubwa ya elimu kwa watoto wa kike shirika hilo limeamua kufanya hivyo ili kuunga mkono ufanisi wao wa kitaaluma katika kuwaandaa waje kuwa na faida kwa jamii na taifa kwa siku za usoni kupitia elimu kwani wataleta mapinduzi chanya katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake Afisa Mwelimishaji Jamii Madhara ya Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuel Goodluck amewataka wanafunzi hao kujitambua na kusoma kwa bidii kusudi wafikie ndoto zao, ambapo pia amewahimiza kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya Ukatili wa Kijinsia ikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji kwani vitendo hivyo vinamadhara makubwa kwa Ustawi wao wa kitaaluma na kiafya pia.

"Tambueni kwamba ninyi ni viongozi katika jamii na katika taifa letu, someni kwa bidii mnapokuwa shuleni kusudi ndoto zenu zitimie. Elimisheni madhara ya ukatili bila kuogopa ili elimu iwafikie wanajamii, achaneni na vishawishi ambavyo vitawafanya mkatishe masomo yenu watoto wa kike mnamchango mkubwa katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia, Jamii hadi taifa,"amesema Goodluck.

Aidha, Goodluck ameiomba jamii kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwa watoto wa kike kufikia malengo yao, amesema kila mmoja anapaswa kuwajibika kikamilifu kuhakikisha kwamba wanafikia hatua njema. Na iwapo kuna watu wanaobainika kuwakwamisha kwa manufaa yao lazima wafichuliwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Emmanuel Goodluck ambaye ni Afisa Mwelimishaji Jamii Madhara ya Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la HGWT akizungumza na Wanafunzi wa Mirwa Sekondari wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Duniani.
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Butiama, Amani Malima ameiomba jamii kuwapa fursa sawa ya elimu watoto wa kike na wa kiume, huku akiomba watoto wa kike wapunguziwe majukumu wanaporejea nyumbani baada ya masomo kusudi wapate muda mwingi wa kujisomea kama ilivyo kwa watoto wa kiume sambamba na kufuatilia maendeleo yao ya kitaaluma shuleni.

Martha Joseph ni mwanafunzi wa kidato cha tatu Mirwa Sekondari ambapo amelishukuru Shirika la HGWT kwa kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wanaoishi mazingira magumu pamoja na kutoa elimu kuhusiana na madhara ya Ukatili wa Kijinsia, ambapo amesema hatua hiyo itachagiza ufauru wao hususan kwa Watoto wa kike kuhudhuria shuleni wakati wa hedhi.

Mathias Peter ni mkazi wa Kata ya Buhemba ambapo amelipongeza Shirika la HGWT kwa namna ambavyo limekuwa likishiriki kupambana na ukatili wa kijinsia kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu katika mikutano ya hadhara, kutumia michezo na kuonesha sinema, hatua ambayo amesema inawafanya wananchi wengi kutambua madhara ya vitendo hivyo. Huku akiomba Jamii kuunga mkono juhudi hizo na serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news