Maagizo ya Waziri Mkuu kwa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mabalozi wanaoteuliwa kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi wanapaswa kutanguliza maslahi ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema kuwa mabalozi hao wanapaswa kutekeleza falsafa ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuona kazi zilizoratibiwa zinaendelea kutekelezwa kwa uadilifu mkubwa na uaminifu ili ziweze kutoa matokeo chanya katika kila kazi zinazofanyika.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Oktoba 3, 2021 ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma wakati alipokutana na mabalozi saba watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Sweden, Rwanda, India, Ethiopia, Uswisi na Jamhuri ya Korea.

Mabalozi hao na nchi zao kwenye mabano ni Luteni Jenerali Yacoub Mohamed (Uturuki), Grace Olotu (Sweden), Meja Jenerali Richard Makanzo (Rwanda), Anisa Mbega (India), Innocent Shiyo (Ethiopia), Hoyce Temu (Uswisi) na Togolani Mavura (Jamhuri ya Korea).

Waziri Mkuu amesema mabalozi hao wana jukumu la kukuza uchumi wa Tanzania kupitia diplomasia ya uchumi. “Waheshimiwa mabalozi mna jukumu kubwa la kukuza uchumi wetu. Nendeni mkaimarishe biashara na nchi yetu. Muangalie sisi tumefanya nini na tumepungua wapi na je tunaweza kurekebisha vipi,” amesema.

Amesema ili Tanzania iweze kupaa zaidi kiuchumi, inapaswa kukuza sekta ya viwanda hatua ambayo itafanya bidhaa zinazouzwa ziwe ni zile zilizosindikwa. “Mnalo jukumu la kuangalia ni namna gani tunaweza kuongeza uzalishaji na siyo wa mazao ghafi bali yaliyosindikwa. Tunataka tuuze kahawa iliyosindikwa hadi mwisho, na kama ni korosho, tuuze zilizobanguliwa.”

“Tanzania tunataka tuimarishe uchumi wetu wa viwanda. Kuna watu wanadai kuwa viwanda vingi vilivyokuwepo zamani vimekufa, lakini wanasahau kwamba teknolojia imebadilika sana. Kwa hiyo leteni watu kwenye uwekezaji wa viwanda, cha msingi wawe ni wale ambao wana historia nzuri kwenye nchi zao (genuine investors),” amesisitiza.

Amesema Tanzania imedhamiria kufufua mazao ya mkonge, michikichi na mbegumbegu za Mafuta na akawataka watafute wawekezaji makini ambao watakuja kuwekeza kwenye mazao hayo.

“Sambamba na hilo, muangalie uwezekano wa kupata masoko ya mazao yanayozalishwa nchini. Mnapaswa muwe ni kiungo baina ya nchi yetu na hizo nchi mnazoenda kutuwakilisha. Muangalie sisi tuna mazao au bidhaa gani na wao wanaweza kuagiza kiasi gani kutoka hapa nchini.”

Amewataka waangalie ni jinsi gani wanaweza kuinua sekta nyingine kama vile utalii kwa kuitangaza Tanzania huko waendako ili kuvutia watalii wengi zaidi. “Tanzania tuna fukwe nzuri sana kule Zanzibar na kuanzia Tanga hadi Mtwara. “Himizeni wawekezaji wa kujenga hoteli kwenye hizi fukwe ili watalii wakija wakute zile wanazozihitaji,”amebainisha.

Kuhusu wana-diaspora, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wawatambue walioko huko waendako, watambue biashara na kazi zao na wawashawishi wafungue matawi ya kampuni zao huku kwao. Amewataka wasiache kuwapa taarifa za mara kwa mara juu ya mambo yanayofanyika hapa nchini.

“Pia angalieni fursa za masomo katika nchi mnazoenda ili Watanzania wapate fursa za mafunzo ya kitaalamu huko nje. Kumbukeni kuwa lugha yetu ya Kiswahili ina fursa nyingi za ajira kwa Watanzania, hivyo msiache kukitangaza Kiswahili katika nchi zenu,”amesisitiza.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka mabalozi hao waende wakaripoti mara moja kwenye vituo vyao vipya vya kazi. “Mmeshapata maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hayo ndiyo maelekezo muhimu. Nendeni vituoni, muda umeisha. Huu siyo muda wa kwenda kuaga mawaziri. Wako wengi sana. Naamini baada ya kuonana na viongozi wetu wakuu, sasa mko imara,”amesisitiza.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wenzake, Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Luteni Jenerali Yacoub Mohamed alimshukuru Waziri Mkuu kwa nasaha alizowapa na kwamba zimewasaidia kutambua msimamo wa serikali ukoje.

“Tutajitahidi kutekeleza yote uliyotuelekeza kwa kadri ya uwezo wetu. Tunatambua uteuzi huu ni fursa kubwa na unaonesha imani aliyonayo Mheshimiwa Rais kwetu. Jambo kubwa tunaloondoka nalo, ni kuweka mbele maslahi ya Taifa letu,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news