Makachero wanasa silaha, madawa ya kulevya

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji , mkoani Pwani linamshikilia mtuhumiwa mmoja jina linahifadhiwa kwa kukutwa na silaha aina ya Rifle yenye No.373 inayodhaniwa kutumika kwenye matukio ya ujangili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, ACP Kungu Malulu amethibitisha kukamatwa kwa mtu huyo katika Kijiji cha Mwangaei Kibata kilichopo Kata ya Kitamba Tarafa ya Kipatimu Wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi.

Ni wakati askari polisi mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa kushirikiana na kikosi cha kuzuia na kupambana na ujangili nchini wakiwa katika msako.

“Walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja mwanaume mwenye umri wa miaka 43,mkulima mkazi wa Mwangei akiwa na silaha aina ya Rifle yenye No. 373 ambayo alikuwa akimiliki kinyume cha sheria na kutumia katika ujangili,"amesema.

Pia amesema katika hatua nyingine walimkamata mtuhumiwa mmoja mwanaume akiwa na silaha aina ya Gobore alilokuwa amelihifadhi juu ya dari la nyumba yakekatika Kijiji cha Kitembo wilayani Kibiti.

Mbali na hayo wamewakamata watuhumiwa wengine wawili wakazi wa Dar es Salaam ambao ni wanaume wakisafirisha viroba vitano vinavyodhaniwa kuwa ni madawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 130.

“Watuhumiwa hawa walikuwa wakitumia gari namba T 559BJL Toyota Corona na watuhumiwa wote wanahojiwa kwa upelelezi na watafikishwa mahakamani,”amesema.

Kamanda Malulu amesema,watuhumiwa wote majina yanahifadhiwa kutokana na sababu za kiupelelezi.

Aidha,Kamanda Malulu ametoa wito kwa wananchi kuzingatia taratibu za kumiliki silaha bila kutumia pasipo uhalali na wale wanaomiliki kihalali wahakikishe wanazingatia matumizi sahihi ya silaha zao.

Post a Comment

0 Comments