Mwanaume wa miaka 37 mbaroni kwa kumuoa mtoto wa miaka 11, nguruwe, fedha zatumika kulipa mahari

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kennedy Fumpa (37) mkazi wa Kitongoji cha Mabatini katika mji mdogo wa Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kumuoa mtoto wa miaka 11 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu Shule ya Msingi Kipundukala.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mabatini, Godfrey Kalungwizi walipata taarifa za utoro wa mwanafunzi huyo na ndipo jitihada za kumtafuta zilianza na baadae walibaini kuwa mwanafunzi huyo ameolewa, baada kuozeshwa na Bibi yake waliyekuwa wakiishi naye kwa kupewa fedha na nguruwe mmoja.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa, kwa taarifa walizonazo ni kuwa mwanafunzi huyo anayeishi na Bibi yake katika kitongoji hicho aliozwa na bibi yake kwa gharama ya sh. 400,000 na ndipo mwanaume huyo alipotoa sh.330,000 na kuongeza nguruwe mwenye thamani ya sh.70,000 ili kuweza kukamilisha kiwango hicho cha sh.400,000.

Amesema kuwa, baada ya mwanaume kukamilisha kiwango hicho cha mali hasa baada ya kukabidhiwa nguruwe alikabidhiwa mtoto huyo wa kike na kwenda kuishi naye kindoa kinyume cha sheria.

Josephat ambaye ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Kipundukala amekiri kuwa, binti huyo ni mwanafunzi wake wa darasa la tatu na alitoweka shuleni hapo kwa muda na kuhesabika kama mtoro na kuwa jitihada za kumtafuta zilikuwa zikiendelea bila mafanikio hadi pale alipopata taarifa za kukamatwa mwanaume huyo akiwa amemuoa mwanafunzi wake.

Peter Lijualikali ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa mtuhumiwa huyo sasa anashikiliwa na polisi na kinachoendelea ni kukamilisha uchunguzi na Jumatano ijayo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo za kuishi na mwanafunzi kindoa kinyume cha sheria.

Mheshimiwa Lijualikali amedai kuwa, ni kitu kisichokubalika kubadilishana mtoto wa kike na nguruwe na sheria zinazomlinda mtoto zipo hivyo watahakikisha sheria inachukua mkondo katika jambo hilo.

Kwa nyakati tofauti, wakazi wa kitongoji hicho wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, kitendo hicho hakikubaliki na wanaziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka.

Aidha, ili kuhakikisha kuwa haki na ustawi wa mtoto unazingatiwa nchini,mwaka 2009 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Mtoto (The Law of the Child Act, 2009).

Sheria hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ambayo imekuwa ikilenga kutetea na kupigania haki na ustawi wa mtoto katika kila kona ya Dunia.

Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (The UN Convention on the Rights of the Child (CRC) na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (The African Charter on the Rights and Welfare of the Child).

Aidha, miongoni mwa dhamira kuu ya sheria hii ni kuimarisha ulinzi kwa mtoto kwa kuhakikisha kuwa hakuna aina yoyote ya ukatili unaofanywa dhidi ya mtoto, vilevile kuhakikisha kuwa hakuna unyanyasaji na ubaguzi wowote unaofanywa dhidi ya mtoto.

Licha ya sheria hii kuwepo tangu mwaka 2009, DIRAMAKINI BLOG imebaini kuwa, ni watanzania wachache akiwemo Kennedy Fumpa wanaofahamu juu ya uwepo wa sheria hii, na baadhi yao wamekuwa wakiwafanyia vitendo vya ukatili watoto kwa kisingizio cha kutokufahamu sheria inayomlinda mtoto.

Wengine pia wamekuwa wakidai wanashindwa kuelewa maana halisi ya ukatili dhidi ya watoto kama huu uliotendeka kwa mtoto huyo wa miaka 11.

Ndoa za utotoni ni miongoni mwa changamoto kubwa ambayo inawakosesha faraja watoto wengi hususani katika jamii za wafugaji na wakulima nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news