WAZIRI UMMY AAGIZA WAKUU WA MIKOA KUSIMAMIA VYEMA TRILIONI 1.3/- ZILIZOTOLEWA NA IMF, APIGA MARUFUKU KUSAFIRI NJE YA MIKOA YAO BILA RUHUSA YA RAIS

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Baada ya Serikali kupata mkopo wa shilingi Trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya mapambano dhidi ya Uviko-19 na utekelezaji miradi ya maendeleo wakuu na mikoa nchini na wakurugenzi wa halmashauri wametakiwa kutumia fedha hizo kwa kazi iliyokusudiwa.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 12,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi za wizara hiyo Mtumba jijini hapa.

Aidha, Waziri Ummy amepiga marufuku wakuu hao wa mikoa na wakurugenzi kusafiri nje ya mikoa yao bila kibali kutoka kwa Rais,Makamu wa Rais au Waziri Mkuu lengo likiwa ni kusimamia kwa ukaribu matumizi ya mkopo huo ambao unadhamiria kufanya maendeleo katika nchi.

Akitoa maelekezo ya matumizi ya fedha hizo za IMF, Waziri Ummy amesema,kwa upande wa mamlaka ya Serikali za mitaa wamepatiwa jumla ya shilingi Bilioni 535.6 ambazo zimegawanywa katika maeneo matatu ikiwa ni pamoja na Elimu, Afya na Kuwawezesha wananchi kiuchumi.

"Naelekeza fedha hizo zinazokwenda kwenye elimu niwaombe wakurugenzi na wakuu wa shule kuhakikisha mnasimamia ujenzi wa madarasa na vifaa vyake zikamilike kabla ya tarehe 15,12,2021.

"Wataalamu naomba mfuatilie kwa ukaribu kila hatua, kiukweli kwa hili nitakuwa mkali kweli sitawafumbia macho wale wote watakaoenda kinyume na utaratibu wa fedha hizo, kwani wapo baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakikiuka maagizo,"amesema Ummy.

Katika hatua nyingine amesema kuwa, kwa upande wa Afya wanakwenda kusimika mitambo ya kisasa ya utoaji huduma za kibingwa.

"Kingine niwaombe fedha hizo ziweze kuwawezesha wananchi kiuchumi katika kuboresha miundombinu kwenye maeneo ya wafanyabiashara jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi katika majiji yetu sita ambayo ni Dar es Salaam,Mwanza,Dodoma,Mbeya,Tanga na Arusha,"amesema Ummy.

Hata Hivyo, amelekeza viongozi wote wa mikoa kuhakikisha wanaweka alama katika majengo yote yatakayojengwa kwa mkopo huo wa IMF ili kuonesha utekelezaji wake kwa vitendo na kwamba viongozi watakaoshindwa kufanya hivyo watapelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Post a Comment

0 Comments