NA MWANDISHI MAALUM
SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imesema ina wajibu wa kuwalinda wakulima nchini kwa namna yoyote ile.
Akiwa katika ziara mkoani Katavi, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hayo kufuatia taarifa ya Wilaya ya Tanganyika iliyolalamikia Mamlaka ya Wanyama Pori (TAWA) kuweka alama za mipaka katika misitu ya Tongwe.

Misitu ya Tongwe iliyopo wilayani Tangayika imekuwa ikisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambapo miezi michache iliyopita ilipokea tangazo la serikali linaloeleza misitu hiyo kuwa chini ya usimamizi wa TAWA bila kushirikishwa
Aidha,katika misitu hiyo wilaya imetenga maeneo ya uwekezaji likiwemo kilimo.Naibu Waziri Bashe ameitaka wilaya hiyo kutowatoa wakulima wote ambao tayari wamekwishagawiwa maeneo ya uwekezaji katika kilimo.
"Haiwezekani TAWA kutumia vibaya mamlaka waliyinayo, waliwezaje kuingia na kuweka bikoni bila kushirikisha uongozi wa vijiji, kata au wilaya,"amesema.









Bashe ameeleza kuwa, kitendo hicho ni sawa na kumchonganisha Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wake.
Ameongeza kuwa, suala hilo linahitaji mashauriano zaidi baina ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mali Asili na Utalii hivyo kukataza halmashauri kutowaondoa wananchi waliopo katika maeneo hayo
Aidha, ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika kutenga eneo la ekari 1000 kwa ajili ya kilimo cha mbegu kufuatia mkoa wa Katavi kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbegu ambapo watafiti wa Taasisi za TARI na ASA watashughulikia uzalishaji huo wa mbegu.



Naibu Waziri Bashe alisisitiza umuhimu wa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya kata, halmashauri na wilaya kuhakikisha wanalinda ardhi ya wakulima, kwa kutenga na kupima ardhi ya kilimo, kama ilivyo katika ardhi ya hifadhi, vyanzo vya maji au hifadhi za taifa.
"Kwa kuwa watu wanazidi kuongezeka lakini ardhi haingozeki, hivyo mahitaji ya ardhi ya kulima inaongezeka, ni muhimu sasa kwa halmashauri zetu kutenga na kupima ardhi ya kulimo, kuepusha migogoro inayoweza kutokea baadae, kama inavyohifadhiwa ardhi ya vyanzo vya maji, hifadhi ya misitu au mapori ya akiba, vivyo hivyo ardhi ya kilimo ihifadhiwe," alisema.