Ahukumiwa miaka 10 jela kwa wizi wa doti 51 za kanga, mapambo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKAZI wa Mboriborini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jijini Zanzibar, Shaabani Abass Rajab mwenye umri wa miaka 27 amepelekwa Chuo cha Mafunzo (jela) kwa muda wa miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba doti za kanga huko Jumbi.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Khamis Simai wa Mahakama ya Mkoa Mwera baada ya Mwendesha Mashitaka, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Safia Serembe kuwasilisha jadala la mshitakiwa mbele ya Mahakama.

Hakimu Khamis ameieleza Mahakama kuwa, ametoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo kwa kuwa kesi za aina hiyo zimekuwa nyingi.

Akiwasilisha jalada la shauri hilo, Wakili Serembe alieleza kuwa Shaabani Abass Rajab alitenda kosa la kuvunja nyumba na kuiba ambapo Novemba 13, 2020 majira ya saa 6:43 mchana Jumbi mshitakiwa huyo alivunja nyumba ya Amour Salim Mohamed kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi.

Kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 292 (1) cha Sheria namba 6 ya mwaka 2018 Sheria ya Zanzibar ambapo kosa la pili siku hiyo hiyo mshitakiwa huyo alitenda kosa la wizi wa kompyuta mpakato moja aina ya Asus rangi nyeusi yenye thamani ya shilingi 400,000 mali ya Amour Salim.

Wakili huyo amedai kuwa, jambo hilo ni kosa kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 251 (1) (2) na 258 vya sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.
Katika kosa la tatu mshitakiwa huyo siku hiyo hiyo aliiba doti 51, vitambaa viwili, pete tatu,hereni za dhahabu peya moja yvenye thamani ya shilingi 1,800,000 mali ya Khadija Kesi Mohamed.

Hata hivyo, awali mshitakiwa huyo aliposomewa kosa lake hilo alikubali ndipo Mahakama ilipoamua aende Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miaka mitano ikiwa ni kosa la kwanza la wizi, na kosa la kuvunja miaka mitano ambapo atatumikia Chuo ha Mafunzo kwa muda wa miaka 10 na adhabu ziende sambamba ili iwe fundisho kwa watu wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.

Post a Comment

0 Comments