BILIONI 1.2/- ZA MIKOPO ZAMIMINIKA TAMASHA LA NJOMBE YA MAMA SAMIA

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Halmashauri ya Mji Njombe imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.2 kwa vikundi 116 vya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu.
Ni kupitia makabidhiano yaliyofanyika katika Uzinduzi wa Tamasha lijulikanalo kama Njombe ya Mama Samia lililoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Gwakisa lengo kuu ikiwa ni kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo.

Sambamba na wilaya kusogeza huduma karibu na Wananchi kwa kutatua kero zikiwemo ardhi na mirathi.

“Tamasha hili litakuwa kwa muda wa siku tatu lengo kuu ikiwa ni kumshukuru Mheshimiwa Rais kwani kwa kipindi cha muda mfupi na nje ya bajeti Wilaya ya Njombe tumepokea kiasi cha shilingi Bilioni 2.8 fedha za UVIKO na Shilingi Milioni 825 ikiwa ni fedha za tozo. Mheshimiwa Rais alituelekeza sisi viongozi kuhakikisha kuwa tunatatua kero za Wananchi. Tutakuwa na jopo la Wanasheria zaidi ya 20 kusikiliza na kutatua kero za Wananchi,”alisema Mkuu wa Wilaya.

Aliendelea kusema, “Kupitia tamasha hili pia Halmashauri ya Mji Njombe inatoa hamasa kwa Wanawake,Vijana na Watu wenye ulemavu kunufaika kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya Wanawake.Vijana na Watu wenye Ulemavu na hii ikawe chachu kwa jamii kujiunga kwenye vikundi na kufanya shughuli za kiuchumi ili kuweza kunufaika na fursa hizo”

Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hizo kwenye Tamasha la Mama Samia, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya amewataka Wananchi katika maeneo inakotekelezwa miradi hiyo kuhakikisha kuwa wanashiriki ipasavyo katika kulinda na kutoa taarifa zenye viashiria vya wizi na amewataka Wafanyabiashara kuleta vifaa vyenye ubora unaotakiwa na kutopandisha bei bila sababu ya msingi jambo ambalo linaweza kupelekea kutokamilika kwa miradi kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.

Aliendelea kusisitiza kuwa Serikali haitakuwa tayari kuvumilia yeyote atakayeshiriki kutumia vibaya fedha hizo zilizoelekezwa kwenye miradi hiyo ya afya na elimu.

“Wito wangu kwa wanavikundi waliopokea fedha hizo kuhakikisha kuwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuinua hali ya uchumi ya Wanakikundi na kuhakikisha kuwa wote waliopokea wanawajibu wa Msingi wa kurejesha ili na wengine wapate fursa ya kukopa. Dawa ya deni ni kulipa,"amesema Mkuu wa Mkoa.

Katika hatua nyingine hamasa imeendelea kutolewa kwa jamii kwa kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 na kuhamasisha Wananchi ambao hawajachanja kwenda kuchanja na kutosikiliza upotoshaji kwa ambao hawajachanja ambapo kwa upande wa Halmashauri ya Mji Njombe,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Erasto Mpete aliongoza zoezi la chanjo kwa kuchanja na kudhihirisha kuwa zoezi hilo la uchanjaji ni endelevu kwa ambao hawajachanja.

Tamasha hilo linalofanyika kwa muda wa siku tatu katika viwanja vya stendi ya zamani Njombe na kushereheshwa na wasanii mbalimbali lenye kauli mbiu ya Njombe ya Mama Samia ni la kipekee na Wananchi wemempongeza Mkuu wa Wilaya na Ofisi yake kwa uratibu wa Tamasha hilo kwani licha ya kutatua kero na kusogeza huduma karibu na Wananchi pia litasaidia kuiweka Njombe kwenye uso wa dunia.

Post a Comment

0 Comments