CCM yamaliza kazi yake mgombea Ngorongoro, Shinyanga Mjini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Taifa imemteua, Emmanuel Lekishon Shangai kuwa mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya chama hicho Jimbo la Ngorongoro katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Desemba 11,2021.

Wakati huo huo kamati hiyo imemteua Gulamhafeez Mukadam na Ella's Masumbuko kugombea kiti cha umeya katika Manispaa ya Shinyanga Mjini.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Shaka Hamdu Shaka kupitia taarifa aliyoitoa leo amesema kuwa, kamati hiyo imekutana katika kikao maalum leo Novemba 7,2021 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Chama cha CCM na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema, uteuzi huo wa Shangai umekuja kufuatia kifo cha marehemu William Tate Ole Nasha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Shaka amesema kuwa,kamati hiyo imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya ujenzi wa Taifa kiuchumi,kijamii na kisiasa.

Aidha, amesema kamati hiyo imempongeza Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja tangu kuingia madarakani kuwa Rais wa Nane wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kuendeleza mshikamano,kuimarisha tunu ya umoja ,amani,utulivu na utekelezaji makini na imara wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.

Post a Comment

0 Comments