Juma Duni Haji kuwania uwenyekiti ACT Wazalendo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imekutana kwenye kikao chake cha kawaida mkoani Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine, kikao hicho cha pili kwa ukubwa kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho kimetoka na maazimio ya kutangaza rasmi uchaguzi wa nafasi za Mwenyekiti wa Chama Taifa, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, na nafasi moja ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama Taifa, nafasi hiyo imetangazwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama Taifa, marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki Februari 17, 2021 na nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar imetangazwa kufuatia kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar,Juma Duni Haji.

Kwenye barua yake ya kujiuzulu aliyomwandikia Katibu Mkuu wa chama Oktoba 30, 2021,Juma Duni Haji ameweka wazi kuwa amejiuzulu nafasi hiyo kwa sababu ana nia ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa chama Taifa, hivyo amejiuzulu ili nafasi hizo mbili zitangazwe pamoja.

Uchaguzi wa Mwenyekiti wa chama, Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar na uchaguzi wa nafasi moja ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ambayo nayo ipo wazi utafanyika kupitia Mkutano Mkuu wa chama Taifa utakaofanyika Januari 29,mwakani.

Post a Comment

0 Comments