Kisa ukosefu wa maji, umeme wanakijiji waanza kuhama kijiji

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WANANCHI wa Kitongoji cha Nambanje kilichopo Kijiji cha Mbimbi katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamedhamiria kuhama kijiji kutokana na sababu ya kukosa huduma ya maji na umeme katika mji wao kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbimbi, Yustus Nyoni ameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, kitongoji chake kimoja kinachoitwa Nambanje katika kijiji hicho wananchi wake wamedhamiria kuhama kijiji hicho kutokana na kukosa umeme na maji katika kitongoji chao kwa muda mrefu huku vitongoji vingine vikiwa na huduma hizo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nambanje, Batlazali Ngonyani amedai kuwa, wananchi wa kitongoji chake walikubaliana katika kikao cha kitongoji hicho kuwa wahame kijiji hicho na kwenda Kijiji cha Namabengo ili waweze kupata huduma muhimu za maji na umeme kama wananchi wengine.
Ngonyani amesema, malalamiko yao ya kudai umeme na maji ni ya muda mrefu, lakini hakuna kinachoendelea kwa sasa na ndipo wananchi wa mji huo kwa pamoja na katika kikao chao cha kitongoji walikubaliana kuhama Kijiji cha Mbimbi na kwenda Kijiji cha Nambabengo.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Salum Nachundu pamoja na kukiri kuwa kitongoji hicho kukosa maji alidai miundombinu ya maji iliharibiwa na mkandarasi aliyekuwa anatengeneza barabara ya Namabengo kwenda Mbimbi na kilichotakiwa kijiji kufuatilia fidia kwa mkandarasi aliyeharibu miundombinu hiyo na kuirudisha kama mwanzo ili wananchi wa kitongoji hicho waweze kuendelea kupata maji.

RUWASA NI NINI?

Sheria Na.5 ya mwaka 2019 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, pamoja na mambo mengine, ilianzisha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambayo ilichukua majukumu yaliyokuwa hapo awali yamekabidhiwa kwa OR-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Majukumu yaliyohamishwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za maji zinapatikana kwenye jamii za watu waishio maeneo ya vijijini, miji midogo na Makao Makuu ya Wilaya.

Sheria Na.5 ya mwaka 2019 imehamisha uwajibikaji wa maafisa wanaohusika na utoaji wa huduma ya maji kutoka OR-TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa (RSs) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda Wizara ya Maji.

Wakala mpya iliyoanzishwa (RUWASA) ina ofisi ngazi za Makao Makuu Dodoma, Mikoa na Wilaya. Hii ni tofauti na muundo wa hapo awali ambao ulikuwa unajumuisha ofisi katika ngazi ya Serikali za Mitaa (LGAs) na Sekretarieti za mikoa (RSs).RUWASA ilianza kazi Julai Mosi, 2019 na mpaka sasa wakala hii inahudumia mikoa 25 ya Tanzania Bara isipokuwa Dar Es Salaam.

Aidha, Nachundu ambaye pia ni mlezi wa Kata ya Litola na fundi mfuatiliaji wa kata hiyo alidai kitongoji hicho kinakosa maji kutokana na bomba linalopeleka maji katika kitongoji hicho kukatwa na mkandarasi aliyekuwa anatengeneza barabara ya Namabengo mpaka Mbimbi.

Mtendaji wa Kijiji cha Mbimbi, Bernadeta Luambano pamoja na mambo mengine amethibitisha kuwa, wananchi wa kitongoji cha Nambanje wanahitaji kuhamia kijiji cha Namabengo kutokana na kukosa maji na umeme katika kitongoji chao.

Kwa mujibu wa Meneja wa Shirika la Umeme nchini (TAMESCO) Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Philipo Joseph Komu alidai kitongoji hicho hakijafanyiwa upembuzi yakinifu na akakiri kupokea malalamiko ya wananchi wa kitongoji cha Nambanje yaliyowasilishwa kwake na mtendaji wa kijiji cha Mbimbi.

Kitongoji cha Nambanje kimepitiwa na nguzo za umeme kutoka kijiji cha Namabengo, lakini kitongoji hicho hakijapata umeme huku vitongoji vingine vya kijiji cha Mbimbi vimepatiwa umeme na kuibua hasira baada ya kuona umeme umepita katika maeneo ya kitongoji chao, lakini wakiishia kuutazama ukipita na kutumiwa na vitongoji vingine vya kijiji chao.

Aidha, Kijiji cha Mbimbi kipo katika Kata ya Litola kikiwa na vitongoji sita na kati ya vitongoji hivyo vitongoji vitano vimepatiwa huduma ya umeme na maji, lakini kitongoji cha Nambanje pekee katika kijiji hicho kimekosa huduma ya maji na umeme na kufikiria kuhama kijiji hicho ili kwenda Namabengo kufuata huduma za maji na umeme wa uhakika kwa ajili ya kufanikisha shughuli zao za maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news