Mbunge Kunambi aneemesha vikundi vya vijana, watu wenye ulemavu, wanawake jimboni

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MBUNGE wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi amekabidhi hundi yenye thamani ya Shilingi Milioni 918 kwa vikundi 100 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu pamoja na kukabidhi Pikipiki 20 zenye thamani ya Shilingi Milioni 50 kwa vikundi viwili vya vijana ikiwa ni sehemu ya mkopo uliotolewa kwa vikundi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo na pikipiki hizo, Mbunge Kunambi amewataka Wanawake, Vijana na wenye Ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo isiyo na riba inayotokana na asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri.

Kunambi amesema kupitia mikopo hiyo wananchi wengi wataweza kuimarisha vipato vyao na kuchochea maendeleo jambo ambalo limepelekea Halmashauri hiyo ya Mlimba kuongoza kwa makusanyo ya mapato kwenye robo ya kwanza katika Mkoa wa Morogoro ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo sambamba na kushika nafasi ya saba Kitaifa.
"Niipongeze sana Halmashauri yetu inayoongozwa na Mkurugenzi wetu Mhandisi Kaliwa ambapo kwa pamoja akishirikiana na sisi Madiwani tumeweza kutenga Sh Milioni 275 na kukusanya Sh Milioni 643 ikiwa ni fedha za marejesho ya mkopo wa miaka ya nyuma na jumla yake ndio unapata Shilingi Milioni 918 ambazo leo tunazikabidhi kwa wananchi wa Mlimba.

"Niwapongeze wananchi wangu wa Mlimba kwa kuwa waaminifu na kurudisha kwa wakati mnapochukua mikopo hii kwani inasaidia kuwezesha vikundi vingine navyo kupata, kupitia mikopo tunaenda kufungua uchumi wa Mlimba na kuimarisha maisha ya wananchi wetu, kwetu ni Historia kubwa kukabidhi hundi yenye thamani hii katika Halmashauri yetu, haijawahi kutokea,” Amesema Mbunge Kunambi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Mhandisi Stephano Kaliwa amesema kuwa Halmashauri hiyo imekua ikitenga kila mwaka asilimia hiyo na kuipeleka kwa walengwa kama mkopo ili kuinua hali zao za kiuchumi na kijamii.

"Pamoja na upelekaji wa mikopo hii Halmashauri itahakikisha kuwa fedha hizo zinarejeshwa kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba,”amesema Mhandisi Kaliwa.

Mkopo huo wa Sh Milioni 918 umetolewa kwa vikundi 69 vya Wanawake vyenye mkopo wa Sh Milioni 570.5, vikundi 29 vya vijana vyenye mkopo wa Sh Milioni 339.5na vikundi viwili vya walemavu vyenye mkopo wa Sh Milioni Nane

Post a Comment

0 Comments