Messi ashinda tuzo ya Ballon d’Or mara saba, Alexia Putellas ang'ara kwa mara ya kwanza

NA GODFREY NNKO

LIONEL Messi ameshinda kwa mara ya saba tuzo ya Ballon d’Or huku Alexia Putellas akishinda tuzo hiyo kwa upande wa wanawake maarufu kama Ballon d'Or Féminin (Women's Ballon d'Or).
Tukio hilo la kihistoria limefanyika Novemba 29,2021 katika Ukumbi wa The Théâtre du Châtelet uliopo jijini Paris, Ufaransa.

Messi ambaye ni nyota tegemeo katika Klabu ya Paris St-Germain na timu ya taifa ya Argentina, taji hilo linamfanya kuweka rekodi ya aina yake tangu aanze kujikita katika soka la ushindani.

Tuzo hii ya 2021, ni maongezeko ya tuzo alizopata za namna hiyo kati ya mwaka 2009,2010, 2011, 2012, 2015 na 2019.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 34 aliisaidia timu ya Argentina kutwaa ubingwa wa Copa America likiwa ni taji la kwanza kwake kubwa ngazi ya taifa, lakini pia alifunga jumla ya magoli 40 akiwa na waajiri wake Barcelona 28, PSG nne na Argentina nane kwa mwaka huu wa 2021 pekee.
Kabla ya kuingia kandarasi ya miaka miwili na PSG hivi karibuni, Lionel Messi ambaye alizaliwa na kukulia nchini Argentina alihamia nchini Uhispania na kujiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka 13.

Nyota huyo aliichezea klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 20 tangu alipojiunga nayo kwa mara ya kwanza Oktoba 17,2004.

Messi akiwa ndani ya klabu hiyo aliendelea kujiimarisha kama mchezaji muhimu wa klabu ndani ya miaka mitatu iliyofuata.

Aidha, katika msimu wake wa kwanza bila kukatizwa mwaka 2008/2009 aliisaidia Barcelona kufanikiwa kushinda mataji matatu ya soka nchini humo na akiwa na umri wa miaka 22 alishinda tuzo yake ya kwanza ya Ballon d'Or.
Nyota huyo, aliendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika misimu ambayo ilifuata, kwani aliweza kushinda Ballons d'Or nne mfululizo.

Ushindi huo ulimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo mara nne mfululizo. Katika msimu wa 2011/2012, aliweka rekodi za La Liga na UROPA kwa mabao mengi yaliyofungwa katika msimu mmoja, huku akijitambulisha kama mfungaji bora wa wakati wote wa Barcelona.
Misimu miwili iliyofuata, Messi alimaliza wa pili kwa tuzo ya Ballon d'Or nyuma ya Cristiano Ronaldo kabla ya kupata hali yake bora kimchezo katika kampeni ya 2014/2015, kuwa mfungaji bora wa muda wote La Liga na kuongoza Barcelona kushinda mataji matatu kwa mara ya pili.

Aidha, baada ya hapo alipewa tuzo ya tano ya Ballon d'Or mwaka 2015, alishika unahodha wa Barcelona mwaka 2018 na 2019 alishinda tuzo ya sita ya Ballon d'Or, hivyo ya sasa inakuwa ya saba.

Wakati huo huo, mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski ameshika nafasi ya pili huku kiungo mkabaji wa Chelsea,Jorge Luiz Frello Filho Cavaliere OMRI (Jorginho) akishika nafasi ya tatu na fowadi wa Real Madrid, Karim Benzema akiwa wa nne katika mfuatano wa kura.
Matukio katika picha yakionyesha hafla hiyo ilivyokuwa. (Picha zote na Ballon d'Or).

Naye nyota wa Manchester United na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo ameshika nafasi ya sita kwenye orodha ya wachezaji waliopata kura nyingi.

Huu unatajwa kuwa ni mwendelezo wa mdororo wa kimafanikio kwa staa huyo wa zamani wa Real Madrid na Juventus ya Italia ambaye anaendelea kusalia na Ballon d’Or tano.

Tuzo ya Ballon d’Or huamuliwa na kura 180 za waandishi wa habari duniani kote ambao hupiga kura za kuamua nani awe mchezaji bora katika kipindi fulan ambapo kutokana na janga la Virusi Vya Korona (UVIKO-19) tuzo hizo mwaka 2020 hazikutolewa ikiwa ni hatua ya kujiadhari kuepuka kusambaa kwa virusi hivyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news