Mwanasheria Mkuu wa Serikali atoa maelekezo kwa wakuu wa idara,vitengo

NA MWANDISHI MAALUM

WAKUU wa Idara na Vitengo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wametakiwa kuweka malengo pamoja na kuwa na miongozo ya ndani itakayoainisha shabaha na muda wa kutekeleza kila kazi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi ( hawapo pichani) katika kikao cha baraza hilo kinachofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jengo la TMDA mkoani Mwanza. Moja ya mambo aliyoyasisitiza ni pamoja na uboreshaji wa maslahi ya watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi zake. (Na Mpigapicha Maalum).

Ametoa wito huo katika siku ya kwanza ya mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unaofanyika jijini Mwanza.

Dkt. Feleshi amesema, Kupitia kikao hicho cha Baraza angependa kukitumia kukumbushana mambo machache kuhusu utendaji kazi wetu wa kila siku katika maeneo kadhaa.

Eneo la kwanza ambalo Mwanasheria Mkuu amewakumbusha wakuu hao wa Divisheni na Vitengo na watumishi wote wa ujumla, ni kuhusu majukumu yetu ya kazi ambapo amesisitiza kwamba ni wajibu wa kila mtumishi kuzitambua na kuzianisha kazi, kuzielewa na kuzitekeleza kwa weledi.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anasema Uzoefu unaonyesha kuwa watumishi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea.

Eneo la pili ambalo Dkt. Feleshi amelikumbusha ni kwa wakuu Divisheni na Vitengo kuweka malengo ya kazi.

“Ninatoa wito kwa Wakuu wa Divisheni na Vitengo kuweka malengo, kuwa na miongozo ya ndani kwa kuanisha shabaha na muda wa kutekeleza kila kazi kwa ufanisi na kwa wakati,"amesisitiza Dkt. Feleshi.

Aidha amebainisha kuwa, Wakuu wa Divisheni na Vitengo wanatakiwa kuhakikisha uwepo wa mambo matatu wakati wa kutekeleza mpango kazi wa Ofisi.

Ameyataja mambo hayo kuwa ni; kueleweka kwa majukumu ( clarity), kwamba kiongozi ahakikishe kazi inayotolewa maelekezo na aliyempa kufanya kazi hiyo anaelewa nini anatakiwa kufanya.

Jambo la pili ambalo ameelekeza kwa wakuu wa divisheni na vitengo kuzingatia ni; uwezo au umahiri( competence) kwamba, mtumishi anayepewa kazi anao uwezo wa kuielewa na kuitekeleza kazi hiyo kwa ukamilifu pasipo makosa.

“Jambo la tatu ni mazingira wezeshi ( Climate) kwamba, pawepo na mazingira wezeshi na yenye kumwezesha mtumishi kufanya kazi zake kwa ufasaha na kufikia malengo yaliyokusudiwa hii ni pamoja na kuwepo kwa vitendea kazi,” amebainisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Eneo la Tatu ambalo amewakumbusha Wakuu wa Divisheni na Vitengo pamoja na watumishi wote ni suala la uadilifu ambapo pamoja na kutilia mkazo kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, lakini amehimiza kutumiwa kwa njia ya kuelimishana na kuchuka hatua stahiki mapema kwa watumishi wenye viashiria vya kutekeleza majukumu yao kinyume na maadili.

“Ofisi iwe ni sehemu ya malezi na siyo kusubiri kutibu tatizo, aidha uzingatiaji wa uadilifu tuuhimize pia kwa Taasisi ambazo ni wadau wetu wa ndani ya nje ambao tunafanya nao kazi,"amesema.

Aidha Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia amesisitiza haja na umuhimu wa kujenga uwazi katika mifumo yetu ya kutekeleza majukumu na vilevile kuomba mrejesho kutoka kwa wadau.

Kuhusu Maslahi ya Watumishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kwamba, amekwisha kutoa maelekezo kwa Menejimenti ya Ofisi kuandaa andiko la kujenga hoja ili Bajeti ya Ofisi yetu na Taasisi zake ziweze kuongezwa na kuwezesha kutatua changamoto zilizopo katika maeneo ya ununuzi wa vitendea kazi, kuboresha maslahi kwa watumishi na mafunzo kwa watumishi.

“Hivyo natoa wito kwa Idara zinazohusika na kazi hiyo kukamilisha kazi hiyo ambayo pia iliridhiwa na kikao cha ( Government Legal Team) kilichofanyika Novemba 22, 2021 ili tuweze kuwasilisha andiko hilo kwenye mamlaka husika,”amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akielezea zaidi kuhusu maslahi ya watumishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa na haya ya kusema

“Kulingana na hali ya kifedha tunayopokea katika Ofisi, hatuna budi tuendelee kutoa kipaumbele kulipa stahiki za watumishi, kwani kwa kulipa madai na stahiki zao mbalimbali kwa wakati tutakuwa tunatekeleza matakwa ya kisheria,”amesema.

Katika siku ya kwanza ya Baraza, wajumbe walipata nafasi ya kupokea taarifa mbalimbali na kisha kuzijadili na pia kutolewa ufafanuzi Makamu Mwenyekiti wa Baraza Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Longopa na Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na Wasimamizi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoka mikoa Tisa ambako Ofisi hizo zipo.

Post a Comment

0 Comments