Mwijaku:Simba SC tunahujumiwa, fedha zinatumika lakini...

NA GODFREY NNKO

Mhamasishaji wa Wekundu wa Msimbazi, Simba SC,Burton Mwambe maarufu kwa jina la Mwijaku amesema kuwa, kuna watu wanaifanyia hujuma timu yao, lakini wanahitaji muda kila kitu kitaisha.
Ameyasema hayo Oktoba 31, 2021 muda mfupi baada ya Wekundu wa Msimbazi kukosa alama tatu dhidi ya Coastal Union katika mtanange uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Mwijaku ambaye pia amejipa cheo cha DC wa Instargram amesema kuwa, "Kuna watu wanakuja hapa wanaifanyia hujuma timu yetu, tujipe muda kila kitu kitaisha tu nawahakikishia.

"Kila timu unayoiona ligi kuu, ujue ni timu kubwa, na niwaambie kila timu inayokuja hapa kuna watu ambao wamejiandaa kuifanyia hujuma timu yetu.Nina uhakika ubingwa upo, ubingwa upo kwa sababu hii ndiyo mechi ya nne sijui ya tatu, kwa hiyo nina uhakika ubingwa tunayo, hii iliyotokea hapa ni sehemu ya mchezo, tuna mechi nyingi zaidi za kucheza, na tutafanya vizuri mimi ninawahakikishia, hizi kelele zitafikia mahali zitaisha zote, tujipe muda tukae karibu na timu na tuisapoti timu yetu, najua watu wanaumia, mashabiki wanaumia, hatuna namna tuipe muda timu, hii timu ni ya kwetu, tunajua...

"Tumeshajua fitina tunazofanyiwa, timu zinazokuja Dar es Salaam hapa huwa zinafanyiwa mambo makubwa sana, yaani kuna watu, kuna wenzetu ambao wamewekeza hela, wewe timu kama hii hapa si ya kulala Golden Tulip, lakini angalia wameenda kulala, watu wanawekeza,"amesema.

Hoja ya Mwijaku inaweza kuwa na mapungufu kutokana na kukosa misimamo thabiti ambayo imekuwa ikionyesha udhaifu katika baadhi ya matamko.

Ni hivi karibuni amegoma kufanya kile alichoahidi kwa mashabiki wa Simba SC mbele ya waandishi wa habari, baada ya kutoa kauli yake ya kwamba angetembea utupu bila nguo, endapo Simba ingepoteza katika mchezo wa marudiano wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Mwijaku alidai kwamba alikua tayari kutekeleleza ahadi yake, lakini alijua kwamba sheria ya nchi haimruhusu kufanya hivyo.

Ikumbukwe klabu ya Simba imeondoshwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu huu na Jwaneng Galaxy ya Botswana baada ya kuruhusu kufungwa bao 3-1 nyumbani kwenye mchezo wa karibuni katika dimba la Benjamin Mkapa.

Hayo yanajiri baada ya Simba kuruhusu kufungwa mabao matatu nyumbani na kufanya uwiano wa mabao kuwa 3-3 baada ya kushinda 2-0 ugenini hivyo kuondolewa kwa kanuni ya bao la ugenini.

Aidha, Simba SC imeonekana kusuasua katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania bara baada ya kutoshana nguvu na Coastal Union, hivyo kulazimika kugawana alama moja moja.

Kwa nini kila mmoja anaitazama Yanga SC?

Ni kutokana na ufundi wao ambao umeonekana kuleta mabadiliko makubwa, mfano jana katika bao la kipindi cha kwanza la mshambuliaji Fiston Mayele dakika ya 36, na lile la kipindi cha pili la Jesus Moloko dakika ya 70 yalitosha kuipa Yanga alama tatu muhimu dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Wakati Simba SC wakiambulia suluhu leo, Yanga ilianza kipindi cha pili kwa kushambulia lango la Azam FC kama walivyoanza mchezo katika kipindi cha kwanza huku umakini kwa washambulia wao Fiston Mayele na Yacouba Sogne ukikosekana baada ya kukosa nafasi kadhaa za kufunga.

Dakika ya 60, kiungo wa Azam FC Sospeter Bajana alikuwa mchezaji wa kwanza kwenye mchezo huu kupata kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi winga mshambuliaji wa Yanga Jesus Moloko.

Azam ilijaribu kufanya mashamhulizi kadhaa ya kutaka kusawazisha bao hilo ila jitihada hizo ziligonga mwamba kutokana na uimara unaoendelea kuonyeshwa na safu ya ulinzi ya Yanga.

Licha ya George Lwandamina kufanya mabadiliko Dakika ya 67, kwa kuwaingiza Ayoub Lyanga na Idris Mbombo ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji ila hawakuweza kuleta madhara yeyote mbele ya mabeki wa Yanga.

Jitihada hizo hazikuweza kufanikiwa mbele ya safu ya ulinzi ya Yanga ambapo dakika ya 70, ilifanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa winga Jesus Moloko na kuendelea kupata matokeo ya ushindi bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa msimu huu.

Dakika ya 73, Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Yacouba Sogne na Jesus Moloko huku nafasi zao zikichukuliwa na Farid Musa na Yusuf Athuman.

Dakika ya 85, Azam ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Never Tigere na nafasi yake kuchukuliwa na Frank Domayo.

Huku kwa upande wa Yanga wakimtoa Feisal Salum 'Fei Toto' na nafasi yake ikichukuliwa na Mukoko Tonombe.

Kipigo hiki kwa Azam FC kinakuwa cha pili msimu huu baada ya Oktoba 2, kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania.
 
Kwa sasa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara watani wao Yanga SC wapo kileleni kwa alama 12, nafasi ya pili ikishikiliwa na Dodoma Jiji FC kwa alama 9, nafasi ya tatu inashikiliwa na Polisi Tanzania FC kwa alama 9 huku Simba SC wakiwa nafasi ya nne kwa alama 8 na nafasi ya tano inashikiliwa na Kagera Sugar FC kwa alama 8.

Post a Comment

0 Comments