Rais Museveni kumkabidhi Rais Samia shule mjini Chato leo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni anatarajia kuwasili wilayani Chato mkoani Geita leo Novemba 29, 2021 kwa ajili ya kumkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Shule ya Msingi Museveni ya mchepuo wa Kiingereza iliyojengwa na Serikali ya Uganda.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameeleza kuwa, shule hiyo ni shule ya msingi mbayo itakuwa inatumia lugha ya Kiingereza.

”Shule hiyo ni shule ya msingi ambayo itakuwa inatumia lugha ya Kiingereza na inategemea kupokea wanafunzi kuanzia shule ya awali na kwenda darasa la kwanza mpaka darasa la saba, mpaka sasa ametujengea madarasa 20 kati ya hayo madarasa 17 ni madarasa kw aajili ya darasa la kwanza mpaka la saba na madarasa matatu ni kwa ajili ya mafunzo ya awali,”amesema RC Senyamule.

Pia ametoa wito kwa wazazi kujitokeza kwa wingi kupeleka watoto katika shule hiyo ambayo inamilikiwa na Serikali ya Tanzania.

”Wananchi wa Geita na Watanzania kwa ujumla jitokezeni kuleta watoto kwenye shule hiyo, tunajua kuwa wazazi wengi huwa wanatumia gharama kubwa kupeleka watoto kwenye shule za lugha ya Kiingereza, lakini shule hii kwa sababu ya kumilikiwa na Serikali na walimu wapo gharama yake huenda ikawa chini kidogo kuliko shule zingine,”amesema RC Senyamule.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, na mgeni wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakisalimiana na wasanii wa vikundi vya ngoma mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Novemba 27, 2021 kwa ajili ya ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini. (Picha na Ikulu).

Post a Comment

0 Comments