Rais Samia atoa maagizo kwa taasisi za fedha nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za kifedha nchini kuja na mapendekezo madhubuti ili kuboresha uchumi na kuongeza uwezo wa kupunguza umaskini kwa haraka hapa nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo Novemba 25,2021 jijini Dodoma.

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Novemba 25,2021 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) unaofanyika kwa siku mbili.

Amesema, Tanzania inaendelea na jitihada za kuzungumza na taasisi za kifedha za Kimataifa kuomba msamaha wa madeni au kurefushwa kwa madeni ili walipe polepole ama kusamehewa madeni.

Pia amesema kuwa, Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi 10 za Afrika zenye uchumi unaokuwa kwa kasi na imeweza kuwa na utulivu wa mfumuko wa bei na utulivu wa thamani ya fedha ukilinganisha na fedha za nchi nyingine.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Samia amesema, mafanikio mengine ni kuonekana kwa viashiria vya maendeleo kwenye maendeleo ya mtu na mtu, kupungua kwa kiwango cha umasikini kutoka asilimia 28.6 mwaka 2015 hadi asilimia 26.2 mwaka 2020.

“Tumeweza kuongeza uhai wa mtu kutoka umri wa kuishi wa miaka 50 hadi 66, lakini kubwa zaidi tumeweza kuingia katika uchumi wa kati mwezi Julai 2020 na tutaendelea kuhakikisha kuwa sera zetu tunazotekeleza zinakwenda kukuza zaidi uchumi wetu ili tusirudi nyuma kutoka katika kiwango ambacho tumefikia.

"Lakini pia mipango yetu ya miaka mitano na yenyewe inaandaliwa katika mifumo ya kupeleka mbele uchumi wetu ili tuweze kuzikabili changamoto zilizopo na tuweze kuzifanyia kazi ili zisiturudishe nyuma,"anesema Rais Samia.

Aidha, amesema mkutano huo umekuja katika kipindi ambacho nchi zote ulimwenguni zinapambana kujitoa kwenye janga la UVIKO 19.

"Kwa hiyo nimefurahishwa na kuona kwamba mada hii itazungumzwa kwenye mkutano huu na nina imani mtajadili haya kwa undani wake na kuona namna kuyafanyia kazi kwenye sera,sheria na mipango yetu ilo tuweze kukuza uchumi wetu.

"Wote tunajua janga la UVIKO-19 ni la kiafya na athari zake ni kubwa katika kila sekta na athari kubwa zimetokea duniani na kwa hapa kwetu tumejitahidi kupambana na kuzuia athari zisitupate kwa wingi na tusiingie kwenye mdororo mkubwa wa kiuchumi,"amesema.

Hata hivyo Rais Samia alisema pamoja na jitihada hizo lakini uchumi wa Tanzania ulishuka hadi kufikia asilimia 4.5 kutoka asilimia 6.8 mwaka 2018/2019 baada ya UVIKO-19 kuingia nchini mwaka 2019/2020 .

Mheshimiwa Rais amesema, Sekta ya Utalii iliathirika kwa kiasi kikubwa zaidi huku akisema mkutano huo uzungumze jambo hilo na kutoka na mapendekezo madhubuti yatakayotumika katika kurejesha haraka uchumi wa Tanzania na kuondoa ama kupunguza kwa haraka umasikini nchini.

"Lakini pamoja na hayo niombe mkutano huu uje na njia ambazo zitasaidia kufaidika na teknolojia ambazo zinatumika duniani hivi sasa pamoja na kuzuia athari kubwa za UVIKO 19 zisiipate nchi yetu,"amesema.

Aidha amesema,kutokana na athari za UVIKO-19 hapa nchini ,Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa chanjo kwa wananchi wake ili kuwalinda, lakini pia kuomba msamaha katika taasisi za kimataifa ili tusamehewe madeni au kuongezewa muda ili yalipwe taratibu. 

"Pia tuliomba kupata fedha zitakazotutoa kwenye athari za UVIKO-19 ambapo tumepata na zimetusogeza mbele,"amesema Rais Samia.

Aliutumia mkutano huo kutoa mwelekeo wa serikali katika sekta ya fedha ambapo alisema Serikali inamalizia sera na mkakati wa kukuza uchumi kidigitali, lakini pia kuongeza nguvu kwenye mambo ya utafiti na ubunifu na Serikali inaendelea kuwekeza kwenye rasilimali watu .
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba,akizungumza wakati wa Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo Novemba 25,2021 jijini Dodoma.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Mwigulu Nchemba amezitaka benki kuwa na ubunifu kusaidia kupata namna ya kutengeneza mipango ambayo itawasaida vijana kupata mitaji.

”Sisi kama wizara tunawakaribisha kuleta kwetu maoni mbalimbali ili hadi tunakwenda bajeti ya pili tuwe na jambo la kisera ambalo tunaweza kulizungumzia,”amesema Waziri Dkt.Nchemba.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof.Florens Luoga akitoa taarifa wakati wa Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo Novemba 25,2021 jijini Dodoma.Awali Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof.Florens Luoga amesema kuwa, mkutano wa mwaka huu ni muhimu kwa sababu wadau wa sekta ya fedha wanaadhimisha miongo minne ya mkutano wa Taasisi za Fedha, tangu kuanzishwa kwake mwezi Mei, 1980.

Prof. Luoga amesema kuwa, mkutano wa Taasisi za Fedha umekuwa jukwaa la wakuu wa taasisi za fedha, wasomi na watendaji kukutana na kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya sekta ya benki, sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla.

“Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, tumeweza kufanya mikutano 19 kujadili masuala mbalimbali, ambayo kwa kiasi kikubwa yaliakisi mahitaji ya wakati huo”amesema Prof. Luoga "Kwa kuzingatia umuhimu wa kukuza uchumi na maendeleo ya teknolojia, tuliona ni vema kuwa na mjadala wa kina kuhusu hatua zinazofaa kuimarisha uchumi na namna ambavyo nchi yetu inaweza kunufaika na maendeleo ya teknolojia,"amesema.

"Mkutano wa mwaka huu unafanyika wakati nchi yetu inatarajia kuadhimisha miaka 60 tangu tupate Uhuru,Desemba 9,1961 hakika nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali. Kwa upande wa uchumi, nchi yetu imeweza kufikia kuwa nchi ya kipato cha kati, mwezi Julai 2020, ikiwa na kipato cha wastani wa dola za Marekani 1,080,"amesema Profesa Luoga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRD ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania, Bw.Abdulmajid Nsekela akitoa salamu wakati wa Mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo Novemba 25,2021 jijini Dodoma.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania, Bw.Abdulmajid Nsekela,amesema kuwa Sekta ya Fedha imejipanga kutumia fursa ya cope26.

”Tunaipongeza Benki Kuu kuja na taarifa rasmi ya kupungiza riba kwa mabenki, hivyo tunaahidi kuwafikia watanzania wengi huku tumejikita kukuza teknolojia ili kuwafikia watanzania,"amesema Nsekela.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news