Rais Samia: Vita dhidi ya ugaidi ni yetu sote

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema Dunia kwa sasa inakabiliwa na tatizo jipya la usalama kwa maana ya ugaidi.
"Kwa hulka ya ugaidi, mtu yeyote bila kujali rangi, dini, umri, itikadi, kipato au uraia anaweza kuwa mhanga wa ugaidi. Mifano ipo nanyi mnaijua, hivyo mapambano dhidi ya tishio la ugaidi si suala la vyombo vya Ulinzi na Usalama peke yenu, bali linahitaji ushirikiano kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Vyombo vya Habari na asasi za kiraia,"ameeleza.

Pia Mheshimiwa Rais amesema kwa sasa hali ya utulivu imerejea katika maeneo ya Mkoa wa Mtwara.

Ni baada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuimarisha ulizi na kukabiliana na tishio la ugaidi.

Amesema kuwa, hivi karibuni kumekuwa na tishio la shambulizi la kigaidi katika mpaka wa Tanzainia na Msumbiji ambapo tishio hilo lilileta hofu kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Kwa mara ya kwanza akiwa amevalia sare za kijeshi, Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na makamanda wa JWTZ cha mwaka 2021 kinachofanyika Lugalo,Dar es Salaam.

Amesema kuwa,  kundi la kigaidi linalotoka katika Jimbo Cabo Delgado nchini Msumbiji lilifanya tishio hilo katika baadhi ya vijiji vya Mkoa wa Mtwara hivyo kufanya wananchi kuwa na hofu huku shughuli za kiuchumi na kijamii zikisuasua.

“Katika kipindi cha hivi karibuni, hali ya ulinzi na usalama wa mipaka yetu hususani kule Kusini ilihatarishwa na tishio la kuwepo kwa kundi la kigaidi linalotoka katika Jimbo Cabo Delgado nchini Msumbiji, kundi hili hujaribu kufanya mashambulizi katika vijiji vyetu vya Mtwara hali inayosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali lakini Jeshi letu limekwenda na linakabiliana na hali hilo.

“Serikali imepeleka vikundi maalumu katika mpaka huo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama, hali iliyosaidia kuleta utulivu na kurejesha shughuli za uchumi na kijamii katika eneo hilo na kupunguza hofu iliyokuwepo,” amesema.

Pia Serikali yake inatambua changamoto mbalimbali zinazolikabili Jeshi hilo na itaendela kuzitatua

“Nayasema haya kuwahakikishia wanajeshi, popote mlipo na Serikali tupo, tunajua katika maeneo ya mipakani kuna changamoto kadhaa, kwa mfano kunakuwa na changamoto za njia kufikia maadui waliko, changamoto ya usafiri, yote tunayajua lakini niwaahidi popote mlipo Serikali tupo,"amesema.

Amewataka makamanda hao wa JWTZ kuliangalia suala la ugaidi na kulijadili katika kikao chao hicho ambacho amakifungua akisema ugaidi ni janga linaloitesa dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news