RC PWANI AONGOZA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA KUDHIBITI VITENDO HARAMU VYA UCHEPUSHAJI MAJI BONDE LA MTO RUVU

NA ROTARY HAULE

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani chini ya mwenyekiti wake, Abubakar Kunenge imeanza kuendesha operesheni maalum dhidi ya kudhibiti vitendo haramu vya matumizi ya maji ya mto Ruvu vinavyosababisha ukosefu wa maji kwa wananchi wanaotumia mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Operesheni hiyo imeanza kufanyika leo katika bonde la mto Ruvu kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo katika Kijiji cha Kidongonzero, Ruvu kwa Dosa,Ruvu darajani na maeneo mengine ya wafugaji.

Kufanyika kwa operesheni ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyotoa mapema wiki iliyopita alipotembelea mtambo wa Ruvu Juu na Ruvu Chini na kutaka shughuli zote za uchepushaji wa maji zinafanyika kando ya bonde la mto Ruvu zisitishwe.

Akiwa katika operesheni hiyo Kunenge ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo ya kupiga marufuku shughuli zote za kilimo,,ufugaji na utumiaji wa mashine kubwa za kuvutia maji katika mto huo zisitishwe maramoja.
Kunenge, amesema kuanzia sasa ni marufuku kwa mkulima yeyote kulima katika bonde hilo kwakuwa watu kama hao wakiachwa wataleta madhara makubwa ya kusababisha upungufu wa maji katika mto huo.

Amesema kuwa,ukiachia kilimo lakini ni marufuku kwa wafugaji kuingiza Ng'ombe zao katika mto huo kwakuwa mifugo hiyo imekuwa sehemu ya kusababisha upungufu wa maji na hivyo kuathiri maisha ya wananchi wa maeneo mbalimbali wanaotegemea kupata maji kutoka mtambo wa Ruvu juu na Ruvu chini.

"Kuanzia leo sitaki kuona shughuli zote za uchepushaji wa maji zinazofanyika ndani ya bonde la mto Ruvu na hata wale wenye vibali kwasasa lazima wasimame mpaka pale Serikali itakapotoa muongozo mwingine,"amesema Kunenge.

Kunenge, ameongeza kuwa kwa yeyote atakayekamatwa kuanzia sasa akifanya shughuli zilizokatazwa katika mto huo atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo ya kufikishwa Mahakamani.
"Wakulima wote wenye vibali na wanatumia maji katika mto Ruvu ni bora wasitishe mapema shughuli zao za umwagiliaji mpaka Serikali itakapotoa ruhusa na wale waliopo ndani ya mita 60 waache kufanya hivyo kwani Serikali inaweka juhudi kuokoa maisha ya Watanzania ili wapate maji huko majumbani kwao,"ameongeza Kunenge.

Kunenge katika hatua nyingine ameamuru maafisa kilimo na mtendaji anayesimamia eneo la Ruvu kwa Dosa wachukuliwe hatua za kisheria kwa kushindwa kudhibiti vitendo haramu vya matumizi ya maji yanayofanywa na baadhi ya wakulima wa bonde hilo.

Kwa upande wake Afisa wa Bonde Msaidizi kutoka Wami na Ruvu, Halima Faraja, amesema toka juhudi na hatua zianze kuchukuliwa maji yameongezeka katika mito hiyo.

Faraja, amesema kuwa hatua mbalimbali bado zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha vitendo vyote vya uchepushaji maji katika mito hiyo vinakomesha ili wananchi wa Pwani na Dar es Salaam waendelee kupata maji kwa uhakika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news