Serikali yatoa maagizo kwa mawakala wa ajira binafsi nchini

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe.Jenista Mhagama amewataka mawakala wa ajira binafsi kuwapatia vipaumbele vijana waliohitimu masomo ya fani mbalimbali na siyo kupeleka wafanyakazi wa ndani katika masoko ya ajira za nje.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa Jenista Mhagama akipata picha ya pamoja na baadhi ya Mawakala Binafsi wa Ajira katika ufunguzi wa kikao na Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini, uliofanyika Novemba 19,2021 jijini Dar es Salaam baada ya kukifungua kikao hicho.

Ameyasema hayo Novemba 19,2021 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao na Mawakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini ili kujadili changamoto mbalimbali ili kuona namna ya kusaidia kupunguza tatizo la ajira.

Amesema,katika kusaidia kupunguza tatizo la ajira, Tanzania ina vijana wengi wenye elimu na hawana kazi ila mawakala hao wamekuwa wakikazana kupeleka wafanyakazi wa ndani.

Amesema, baadhi ya kampuni hazina leseni za kufanya kazi za uwakala wa ajira na baada ya kukaguliwa walibaini kuwa nyaraka walizokuwa wakitumia ni batili, siyo halali ili wajipatie leseni za kufanya biashara za uwakala.

“Tatizo kubwa la ajira ni kwa vijana waliosoma, wahitimu wapo wanamaliza kila siku na tukienda katika hizo nchi tunakuta na watu waliosoma kwa viwango tofauti kutoka nchi nyingine wanafanya kazi kwanini sisi hatuhangaiki na hao tunataka tukawakusanye watu Njombe tuwapeleke huko,”amesema.

Pia ameilekeza ofisi yake kuhakikisha Makampuni ya Uwakala Binafsi wa Huduma za Ajira watakaoomba usajili na ambao wameshaomba wafanyiwe ukaguzi kabla na baada ya kupata usajili ili kubaini mapungufu ya utekelezaji wa Sheria ya Huduma ya Wakala Binafsi wa Ajira Na.9 ya mwaka 1999 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2014.

Amesema, wameimarisha usimamizi wa huduma za ajira kwa kuanzisha na kukijengea uwezo Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) ili kiweze kusimamia na kuratibu ipasavyo utafutaji wa fursa za ajira ndani na nje ya nchi pamoja na michakato ya kuunganisha watanzania na fursa husika.

Pamoja na hayo amesema,Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa shughuli za Wakala wa Ajira ili ziweze kutekeleza shughuli zao kwa weledi na uadilifu na hivyo kuchangia katika kupunguza tatizo la ajira nchini, kukuza uchumi na kuchangia pato la Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya mawakala hao,Bw. Jeremiah Maselle ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya JMaselle Investiment amesema ujio wa waziri eneo hilo utatoa majibu ya matatizo yao ambayo wamekuwa wakiyalalamikia kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news