Serikali yazindua mfumo wa kudhibiti ajali za barabarani

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amezindua mfumo wa maeneo ya udhibiti ajali kwenye barabara (Buffer Zone) kwa waendesha pikipiki.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akitoa cheti kwa dereva wa bodaboda aliyepitia mafunzo maalum ya kusimama pikipiki (bodaboda) wakati taa nyekundu inapowaka barabarani (Buffer Zone). Uzinduzi huo ulifanyika jijini Arusha, Novemba 25, 2021. (Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).

Lengo kuu la uzinduzi wa mfumo huo ni kufanikisha dhamira ya usalama barabarani kwa watumiaji wa barabara, kuboresha matumizi salama ya barabara.

Mfumo huo umezinduliwa mkoani Arusha na unakuwa wa kwanza kwa nchi za Afrika, umedhihirisha kuwa na mafanikio makubwa katika nchi nyingi duniani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Simbachawene alisema mfumo huu siyo tu unaweza kuboresha usalama bali pia unapunguza matukio ya ajali kwa watembea kwa miguu zinazosababishwa na waendesha pikipiki.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa sehemu maalum ya kusimama pikipiki (bodaboda) wakati taa nyekundu inapowaka barabarani (Buffer Zone). Uzinduzi huo ulifanyika jijini Arusha.

“Tuna imani kuwa, kuzinduliwa kwa maeneo haya utafanikisha lengo lililokusidiwa la kupunguza ajali zitokanazo na waendesha pikipiki kwa Jiji letu la Arusha na kuwa mfano wa kuigwa katika maeneo mengine nchini,”amesema Simbachawene.

Aidha, Simbachawene alitoa wito kwa Watanzania akisema kuwa suala la usalama barabarani ni la kila mtu, hivyo ni vyema kuzingatia sheria za barabara na kuepuka kilevi wakati wa kuendesha chombo cha moto.

Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Mhandisi Kashinde Musa, alisema wizara inaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na sera ya usalama barabarani ili kuwapa uelewa watumiaji wa barabara na kuboresha usalama barabarani.

Kashinde aliongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la watumiaji vyombo vya moto hususani waendesha pikipiki ambao pamoja na kuwa na lengo la kurahisisha usafiri hasa mijini umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ajali barabarani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa sehemu maalum ya kusimama pikipiki (bodaboda) wakati taa nyekundu inapowaka barabarani (Buffer Zone). Uzinduzi huo ulifanyika jijini Arusha.

“Tunakusudia pia kuweka mikakati itakayosaidia kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara yenye lengo la kupunguza ajali za barabarani hasa zinazosababishwa na waendesha pikipiki,” alisema Kashinde.

Alisema kuwa mikakati hiyo itahusisha kutenga eneo maalum kwenye makutano ya barabara (Buffer Zone) kwa ajili ya kuratibu vitu waendesha pikipiki ili waweze kuvuka salama katika maungio ya barabara.

Naye Dk. Christina Kayoza ambaye alimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) alisema kuwa TANROADS imekuwa ikifanya juhudi kubwa kwa kujenga miundombinu ya barabara iliyo salama kwa watumiaji pamoja na kuweka alama za barabarani.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia aliyevaa kaunda suti), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa sehemu maalum ya kusimama pikipiki (bodaboda) wakati taa nyekundu inapowaka barabarani (Buffer Zone). Uzinduzi huo ulifanyika jijini Arusha. Katikati ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Khamis Hamza Chilo. na wapili kushoto ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi, Kashinde Musa.

Alisema pia wanatoa elimu kwa watumiaji wa barabara na kuweka mifumo stahiki inayoelekeza matumizi sahihi ya barabara.

Aliongeza kuwa pamoja na juhudi hizo bado kuna changamoto kubwa ya usalama kwa watumiaji wa barabara zinazosababishwa na tabia za madereva wanaoendesha vyombo vya moto.

Alisema kuwa mkakati huu utaongeza nidhamu kwa waendesha pikipiki kwani watatakiwa kutulia kwenye eneo lililokusudiwa na kusubiri mwongozo wa taa za barabarani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Khamis Hamza Chilo, wakati alipokuwa anawasili katika hafla ya uzinduzi wa sehemu maalum ya kusimama pikipiki (bodaboda) wakati taa nyekundu inapowaka barabarani (Buffer Zone). Uzinduzi huo ulifanyika jijini Arusha.

Mradi huo ambao ni wa majaribio utahusisha kutenga eneo maalum litakalokuwa na michoro ya barabara kwa ajili ya waendesha pikipiki katika makutano ya barabara.

Pia itahusisha kuchora alama ya pikipiki kwenye eneo lililotengwa, kutoa namba maalum kwa kila mwendesha pikipiki zitazotumika kuwatamhulisha kwa kubandikwa nyuma ya makoti yao pamoja na kutoa elimu endelevu kwa watumiaji wote wa barabara.

Post a Comment

0 Comments