TANI 30.8 ZA MADINI YA RUBY ZIMECHIMBWA MUNDARARA-WAZIRI BITEKO

NA TITO MSELEM-WM

ZAIDI ya tani 30. 8 za Madini ya Ruby yenye thamani ya shilingi Bilioni 3,165,208,679.80 yamechimbwa katika Mgodi wa Sendeu Agrovet Co. Ltd uliopo wilaya ya Longido Mkoani Arusha.

Jumla ya tani 178.495 za madini yamechimbwa na kufanyiwa uthaminishaji na kubainisha thamani ya madini yaliyochimbwa katika mgodi huo ulioanza uzalishaji Mwaka 2019 kuwa ni shilingi 5,791,347,239.63 hadi kufikia tarehe 5 Novemba 2021.

Leo tarehe 20 Novemba, 2021, Waziri wa Madini, Doto Biteko amefika katika mgodi huo kushuhudia upatikanaji wa madini hayo ambapo ameipongeza kampuni ya Sendeu Agrovet Co. Ltd kwa kupata madini hayo na kuwataka wachimbaji wa Madini ya Ruby kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana.
“Mahali popote penye ridhiki hapakosi migogoro, hivyo Sendeu nikuombe ukae vizuri na hawa watu msigombane mheshimiane na mthaminiane, Rais wetu anataka kuona wachimbaji wanatajirika,” amesema Waziri Biteko.

Waziri Biteko amesema Serikali itaendelea kumuunga mkono mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa Ruby Sendeu Laiza na kumtaka achimbe kwa kufuata Sheria na kuzingatia kulipa Kodi ya Serikali.

Aidha, Waziri Biteko amesema uwepo wa madini ya rudy katika kijiji cha Mudarara ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa Mundarara, wilaya ya Longido na kwa watanzania wote kwa ujumla.
Pia, Waziri Biteko ametoa wito kwa wachimbaji, wafanyabiashara wa madini na wadau wote kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na stahiki ya Serikali.

Kwa upande wake, Mmiliki wa Mgodi wa Sendeu Agrovet Co. Ltd Sendeu Laiza amesema uchimbaji rasmi wa madini ya ruby katika kijiji cha Mundarara ulianza mwaka 1948 ukifanywa na kampuni ya kigeni iliyokuwa imesajiliwa nchini Kenya iliyojulikana kwa jina la Continental Ore Company Ltd.
Sendeu amesema, Baada ya Tanganyika kupata Uhuru mwaka 1961 Serikali ya Tanzania iliutaifisha mgodi huo mnamo mwaka 1973 na kuukabidhiwa kwa Tanzania Gemstone Industries ambayo ni Kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Post a Comment

0 Comments