TCCIA Mkoa wa Mara kuanzisha kampeni maalumu ya kutangaza fursa zilizopo mkoani humo za kiuchumi

NA FRESHA KINASA

MWENYEKITI wa Chama cha Wafanyabiashara Kilimo na Wenye Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara,  Boniphace Ndengo amesema wanatarajia kuanzisha kampeni maalumu ya kutangaza fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo mkoani humo zijulikane zaidi kitaifa na kimataifa ili kuwafanya wawekezaji kutoka mikoa ya ndani na nje waje kuwekeza,  hatua ambayo itachangia kukuza uchumi wa wananchi wa Mara.
Ndengo amesema, Mkoa wa Mara ni Mkoa wenye fursa nyingi ikiwemo utalii, kilimo, idadi kubwa ya mifugo, ardhi bora, Ziwa Victoria pamoja na utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu ambapo amesema kupitia kampeni hiyo ambayo itazinduliwa wiki mbili zijazo itatumika kufikisha ujumbe kwa watu mbalimbali waweze kuzijua kikamilifu fursa hizo na kuja kuzitumia kikamilifu ili zilete mapinduzi chanya ya kiuchumi pamoja na kuwezesha upatikanaji wa masomo ya bidhaa zinazozalishwa na Wajasiramali wa Mkoa huo.

Ameyasema hayo leo Novemba 23, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Musoma ambapo pamoja na mambo mengine amesema, Kauli mbiu ya kampeni hiyo itajulikana kwa Jina la ''Karibu Mara eneo jipya la uwekezaji Biashara na Utalii Ukanda wa Afrika Mashariki'' ambapo shahaba kubwa ni kuifanya Mara kuwa mpya kwa kuitangaza kikamilifu kwa njia ya teknolojia na vyombo vya habari ijulikane zaidi kitaifa na kimataifa.
"Kituo hiki sasa kitatumika pia kutatua changamoto ya masoko na mitaji kwa wajasiriamali taasisi mbalimbali za fedha tutashirikiana nazo kwa Karibu kabisa ili kama kuna changamoto zozote za kibiashara zinazowakabili wajasiriamali na wafanyabiashara zitapatiwa ufumbuzi ili Mara Yetu ipige hatua kwenda mbele kimaendeleo,"amesema Ndengo.

"Nitumie fursa hii kuwaalika wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo waje kutumia fursa hii na wajitokeze kuwekeza. Mara ni mkoa muhimu sana hasa ikizingatiwa unapakana na nchi jirani ya Kenya kupitia lango la Sirari kwa hiyo mkoa tukiutangaza kikamilifu utafunguka na kujulikana zaidi na kusifika kwa mema waone Mara ni lango la Kibiashara,"mesema Ndengo.

"Mara pia ni mkoa wa kihistoria katika Taifa letu. Kutokana na kumtoa kiongozi mahiri na shujaa ambaye pia alifanikisha ukombozi wa nchi nyingi barani Afrika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Hayati Baba wa Taifa) na kuliletea heshima taifa letu, jambo hili pia lazima lisemwe na kutangazwa kupeleka ujumbe sehemu mbalimbali duniani. Ili Mara uwe Mkoa wa Kimkakati na kiuwekezaji kiuchumi," amesema Ndengo.
"Mkoa wa Mara una Hifadhi ya Serengeti na hivyo kuwezesha shughuli za utalii, fursa ya uchimbaji madini pamoja na mazao yanayosafirishwa likiwemo zao la Kahawa na pamba ambapo pia mazao haya katika Mkoa wa Mara yanastawi vyema. Sambamba na idadi kubwa ya mifugo, Ziwa Victoria na ardhi bora yenye rutuba kwa shughili za kilimo, hizi fursa zote ni faida kwa Ustawi wa Maendeleo ya Mkoa wetu na nchi yetu pia.

"Maonesho haya yataanza kufanyika wiki mbili zijazo ndani ya ukumbi wa jengo la NHC la Mukendo Plaza Manispaa ya Musoma wafanyabishara na wajasiriamali watakuwa na bidhaa mbalimbali na pia bidhaa zao zitatangazwa, pia huduma zitatolewa ikiwemo elimu ya biashara, ushauri, maonesho, utamaduni, Kituo Cha Utalii, pia kutakuwa na Kituo cha Habari kila siku habari zitaandikwa kutangaza fursa na vivutio vya Mara na kazi za wafanyabiashara na wajasiriamali wote ili duniani itambue na kuwavuta wawekezaji waje kwa wingi. ambapo bidhaa 100 zitatangazwa," amesema Ndengo.
Katika hatua nyingineingine, Ndengo amesema, TCCIA mkoa huo itaendela kushirikiana na Wafanyabishara na Wajasirimali wote katika kuhakikisha kwamba wanakuwa na umoja wa kuwezesha kusonga mbele na kunufaika na fursa mbalimbali na hivyo akawaomba Wafanyabiashara ambao bado hawajajiunga na TCCIA wajiunge.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news