Waziri Ummy aipa tano Jiji la Dodoma kwa kuvikopesha vikundi

NA DENNIS GONDWE

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza takwa la kisheria kuvikopesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu shilingi 1,039,050,000 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.

Waziri Mwalimu amesema hayo alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Jiji la Dodoma waliojitokeza katika bustani ya Nyerere square kabla ya tukio la kukabidhi mfano wa hundi ya shilingi 1,039,050,000 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Niwashukuru na kuwapongeza sana Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma chini ya Mstahiki Meya, Prof. Davis Mwamfupe. Pongezi hizi ziende hadi kwa watendaji wake chini ya Mkurugenzi, Joseph Mafuru kwa kutekeleza kikamilifu maelekezo ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Si mkopo kiduchu, Jiji la Dodoma mpo juu, hongereni Dodoma," alisema Waziri Ummy kwa furaha kubwa.
Aidha, Waziri huyo alilitaka jiji hilo kuendelea kutoa mikopo mikubwa wa vikundi vya kiuchumi. “Ni matumaini yangu kuwa Jiji la Dodoma haitakuwa mara ya mwisho kutoa mikopo mikubwa. Tunataka kuona mikopo mikubwa, wakopaji wenye mawazo mazuri yanayotekelezeka wapewe mikopo hata milioni 100 na kuendelea. Lakini pia msiache kutoa mikopo midogo kwa vikundi. Najua kuna vikundi ambavyo mnatakiwa kuanza navyo kidogo kidogo kisha vinaenda vinakuwa” alisema Waziri Mwalimu.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa Halmashauri hiyo haijawahi kuwa na upungufu wa fedha. Alisema kuwa upungufu unaoikabili halmashauri hiyo ni vikundi kwenda kukopa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa kwa kipindi cha robo ya kwanza 2021/2022 jumla ya shilingi 1,039,050,000 zimekopeshwa kwa vikundi 48. Alisema vikundi vya wanawake 19, vijana 19 na watu wenye ulemavu 10. Kati ya fedha hizo shilingi 238,514,365 ni mgao wa robo ya kwanza na shilingi 800,535,635 ni fedha zilizovuka mwaka, aliongeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news