Waziri Ummy:Changamoto hazikosekani, miji yetu lazima ipangwe

NA NTEGHENJWA HOSSEAH
 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema changamoto hazikosekani, lakini miji yetu ni lazima ipangwe sambamba na kuwapelekea wafanyabiashara katika maeneo yaliyoandaliwa ili kufanya biashara kwenye mazingira bora.
Waziri Ummy ameyasema hayo alipotembelea Soko la Karikaoo kuangalia maandalizi ya ukarabati wa soko la zamani sambamba na ujenzi soko Jipya la Kariakoo.

“Nimefika leo kwa ajili ya kufuatilia na kutekelezeka maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Soko la Kariakoo.Lazima miji ipangwe, na tunamshukuru Mhe. Rais amesisitiza lazima miji ipangwe na iwe salama, changamoto hazikosekani, lakini tuzitatu,e naupongeza Mkoa wa Dar es Salaam kwa jitihada kubwa za kuwapanga wamachinga.

"Naelekeza fedha zilizotolewa na Mhe. Rais Shilingi Bilioni 32.2 ziombwe na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam sababu mradi huu ni mkubwa na wilaya watakuwa wafuatiliaji wa karibu, lakini Mkoa lazima wasimamie kikamilifu.

“Ninachotaka kuona ni Soko lijengwe kwanza baadae ndiyo tutajua namna ya Menejimenti kama lisimamiwe na Jiji au Shirika la Masoko Kariakoo.

"Soko letu liliungua Julai, tulipeleka maombi kwa Mhe. Rais ya kulikarabati ametukubalia, na ametukubalia kujenga soko lingine kubwa litakalokuwa na ghorofa sita kwenda juu na mbili kwenda chini,”amesema.

Aidha ameagiza Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba fedha hizo kwa Wizara ya Fedha na Mipanho si zaidi ya tarehe 15 mwezi huu ili kazi ianze mara moja, uanze ukarabati wa soko hilo na ujenzi wa soko lingine jipya.

“Soko Jipya litakuwa na wafanyabiashara zaidi ya elfu mbili,vipaumbele ni hivyo wala wafanyabiashara wasiwe na wasiwasi wote watapewa maeneo ya biashara baada ya ukarabati na ujenzi,"amesema.

Post a Comment

0 Comments