Handeni wamfurahisha Waziri Ummy kwa ujenzi wa madarasa kupitia fedha za UVIKO-19

NA RAPHAEL KILAPILO

HALMASHAURI ya Mji wa Handeni imepongezwa kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa madarasa kwa shule za Msingi na Sekondari kwa kutumia pesa za UVIKO-19.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) alipotembelea Halmashauri ya Mji wa Handeni, Desemba 6, 2021 kukagua miradi ya maendeleo.

“Nimefurahishwa sana na ubunifu wenu, tumeleta fedha za madarasa 22 hapa, lakini mkaona kuna kata ipo mbali na haina shule, wananchi wameanza kujenga madarasa yao, kwa hiyo zile hela za UVIKO-19 mkaleta hapa madarasa mawili ili kuwapunguzia umbali watoto wa kata hii ya Malezi wanaotembea takribani kilomita 19 kwenda Handeni Mjini wapate elimu. Jambo hili ni zuri ninawapongeza sana,”amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy alieleza kuwa ameambiwa wanaomaliza kidato cha nne kwa Halmashauri ya Mji wa Handeni ni 1,100 na wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza Januari 2022 ni wanafunzi 1,668 na kuleta ongezeko la wanafunzi 667.

Alieleza kuwa, wanafunzi wote kwa mara ya kwanza historia inaandikwa, wanaenda kuanza shule kwa siku moja ifikapo Januari 17,2022 na kuwataka kukamilisha madarasa 22 ya kidato cha kwanza ifikapo Desemba 15, 2021.

“Mmesema hapa Handeni kidato cha nne wanaacha madarasa 24, lakini halmashauri inaenda kukamilisha ujenzi wa madarasa 22 hivyo kutakuwa na jumla ya madarasa 46 maana yake hakuna mtoto wa Handeni atakayebaki nyumbani kwa sababu amekosa darasa. Hii ni hitoria inaenda kuandikwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan,"alisema Ummy.
Aidha, Waziri Ummy aliwataka wakurugenzi wote kukamilisha ujenzi wa madarasa 12000 yanayojengwa nchi nzima, ifikapo tarehe 15 Desemba, 2021 ikiwa imebaki takribani wiki moja.

Pia Waziri Ummy aliwaagiza wakurugenzi kutumia mapato ya ndani kujenga vyoo vya wanafunzi na wasitarajie kwamba fedha ya kujenga vyoo itatoka Serikali Kuu.

Kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Elimu darasa moja ni lazima liwe na matundu ya vyoo mawili.
“TAMISEMI hatupoi na hatusubiri hivyo msisubiri Serikali Kuu. Sisi tunaleta madarasa, nguvu za wananchi pamoja na Halmashauri mzielekeze kwenye ujenzi wa natundu ya vyoo pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu. Hivyo ni lazima wakurugenzi mjiongeze " alisema Ummy.

Katika shule za kata 214 za Sekondari zinazojengwa nchi nzima Mkoa wa Tanga zinajengwa shule 12 zenye thamani ya shilingi bilioni 5.6 na kwa Halmashauri ya Handeni inajengwa katika Kata ya Mlemani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news