Ligi Kuu Tanzania Bara yazidi kuwa ya moto

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WANAJANGWANI Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi baada ya kuichapa Biashara United ya mkoani Mara mabao 2-1.

Ni katika mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Desemba 26, 2021 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Biashara United walitangulia kwa bao la Atupele Green Jackson dakika ya pili tu ya mchezo, kabla ya mshambuliaji Fiston Kalala Mayele kuisawazishia Yanga SC dakika ya 40.

Ni bao la kipekee ambalo lilitokana na krosi ya Mkongo mwenzake, beki Djuma Shabani kutoka upande wa kulia. 

Kiungo mkongwe Mrundi, Said Ntibanzokiza akaifungia bao la ushindi Yanga dakika ya 79 kwa penalti baada ya beki Abdulmajid Mangaro kumsukuma winga Mkongo, Jeses Moloko Ducapel upande ule ule wa kulia.

Yanga inafikisha alama 26 katika mchezo wa 10 na kuendelea kuongoza ligi kwa alama tano zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi. 

Awali Tanzania Prisons imejikusanyia alama tatu kwa ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar, mtanange ambao ulipigwa katika dimba la Kaitaba mjini Bukoba. 

Bao pekee la Tanzania Prisons ambayo mechi mbili zilizopita ilifungwa 2-1 na Yanga mjini Sumbawanga na 1-0 na Geita Gold mjini Geita, bao lake pekee katika mchezo wa limefungwa na Marco Mhilu dakika ya 78 akimalizia pasi ya Jeremiah Juma.

Kwa ushindi huo katika mechi ya 11, Tanzania Prisons inafikisha alama 11 na kusogea nafasi ya 10, wakati Kagera Sugar iliyopoteza mechi ya pili mfululizo nyumbani kufuatia kufungwa 2-0 na Mbeya Kwanza Desemba 22, inabaki na alama zake tisa katika nafasi ya 13.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news