Mtanzania ni miongoni mwa waliodakwa na makachero nchini Malawi

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Uhamiaji nchini Malawi inawaweka kizuizini Mjini Lilongwe raia wa Tanzania, Wazimbabwe wawili na raia wa Nigeria kwa kukaa nchini humo kinyume cha sheria.
Wahamiaji haramu nchini Malawi. Picha na M24).

Msemaji wa Ofisi ya Uhamiaji Kanda ya Kati nchini humo, Inspekta Pasqually Zulu amethibitisha tukio hilo.

Inspekta Zulu amesema, wanne hao walikamatwa wiki hii wakati maofisa wa Uhamiaji na Polisi walipoendesha operesheni ya pamoja katika wilaya za Lilongwe na Dowa.

Amesema,operesheni hiyo iliyofanyika usiku, ilishuhudia polisi na maafisa wa uhamiaji wakifanya ukaguzi maeneo kadhaa ikiwemo Bwandiro, Wakawaka, Devil Street, Living Room, Falls na Kambi ya Wakimbizi ya Dzaleka huko Dowa.

Inaelezwa kuwa mwanzoni, watu 11 wakiwemo Wachina wawili, Wanyarwanda watatu, Msumbiji mmoja,Mmalawi mmoja, Mtanzania mmoja, Wazimbabwe wawili na Mnigeria mmoja walikamatwa kwa makosa mbalimbali.

Hata hivyo, wakati wa uthibitishaji wa hati na uhalisi wa hali yao ya makazi, saba waliachiliwa lakini walishauriwa kwamba wanapaswa kusafiri kila mara wakiwa na nakala zilizoidhinishwa za hati zao ili kuthibitisha hali yao ya kukaa kisheria nchini Malawi.

Inspekta Zulu amethibitisha kuwa wanne waliosalia bado wapo chini ya ulinzi wa polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayohusiana na kukiuka sheria mbalimbali za Uhamiaji za Malawi.

Wanne hao wametambuliwa kuwa ni Bw. Bilali Muhammed raia wa Tanzania, Bw. Tendai Kaorayi na Bi.Regina Kuwamba wote raia wa Zimbabwe na Bw.Julian Onyeka Ihuoma raia wa Nigeria.

Wakati huo huo, Inspekta Zulu amesema Idara ya Uhamiaji pamoja na polisi, wataendelea kufanya operesheni kwani wahamiaji haramu wote wanatakiwa kukabiliwa na sheria.

"Wahamiaji haramu ni tishio kwa usalama wa taifa na maendeleo ya uchumi wa kijamii wa nchi, kwa vile msimu wa sikukuu unakaribia, maofisa wa Uhamiaji na Polisi watakuwa wakiendesha msako huu wa pamoja," amesema Inspekta Zulu. (Mashirika)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news