Mtanzania Yusuph Kileo atoa angalizo kuhusu uhalifu wa mtandao msimu huu wa sikukuu

NA MWANDISHI MAALUM

MTAALAMU wa Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Digitali nchini, Bw. Yusuph Kileo amehimiza makampuni kuwa na umakini mkubwa kwa kuongeza nguvu kwenye udhibiti wa uhalifu wa mtandao hususan kipindi hiki ambapo wengi wapo likizo na mara nyingi hujisahau. 

Katika sherehe za Krisimasi na Mwaka Mpya pamekuwa na kawaida ya wahalifu wa mtandao kuongeza mashambulizi mtandaoni katika maeneo mengi duniani.
Hii ni kutokana na kampuni nyingi kuruhusu wafanyakazi kwenda nyumbani na wahalifu wanajua ndio muda sahihi, kwani wengi huachana na shughuli za kikazi.

Ndani ya kipindi kifupi tayari matukio yameongezeka, nchini uengereza kampuni ya James Hall & Company, ilipata mashambulizi ya kimtandao yaliyopelekea maduka kadhaa ya Spar kufunga kutoa huduma zake.

Wakati huo huo kampuni ya magari ya Volvo nayo imeripoti kukumbwa na mashambulizi ya mtandao ambapo taarifa kadhaa za kampuni hiyo zilipotelea mikononi mwa wahalifu na tayari imetangaza kufanyia uchunguzi udukuzi huo wa kimtandao.

Kampuni ya Bima ya Lloyd's Insurance nayo imeonekana kutoa tamko rasmi kuwa haitowalipa waathirika wa uhalifu wa mtandao ambao utahusishwa na taifa moja kudhuru taifa lingine kimtandao "State sponsored cyberattack" ambapo kwenye taarifa ya kampuni hiyo wameelezea wasi wasi wao wa kukua zaidi kwa matukio ya kihalifu mtandao yatakayo pelekea hasara kubwa.

Wana usalama mtandao tayari wameanza kuonyesha hofu kuwa mashambulizi ya mtandao yatachochewa zaidi na udhaifu uliogundulika "Log4shell" ambapo inaaminika makampuni mengi duniani yamekuwa yakitumia huduma zake kwenye tovuti pamoja na programu tumishi mbali mbali.

"Mataifa yetu ya Afrika yamekuwa na muamko wa matumizi makubwa ya TEHAMA, tumeona uwekezaji mkubwa kwenye TEHAMA wenye dhamira ya kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma - Ila hatupaswi kusahau kuwa kadri tunavyoendelea kuwekeza kwenye TEHAMA kurahisisha mambo yetu na kuongeza ufanisi ndio hivyo hivyo tunakaribisha matukio zaidi ya kihalifu mtandao". Yusuph Kileo, Mtaalam wa usalama wa mtandao na uchunguzi wa makosa ya digitali anaeleza. 

Kileo amehimiza makampuni kuwa na umakini mkubwa kwa kuongeza nguvu kwenye udhibiti wa uhalifu wa mtandao hususan kipindi hiki ambapo wengi wapo likizoni na mara nyingi hujisahau.

"Wahalifu mtandao huwa hawaendi likizo, na ndio maana tumekuwa tukihimiza makampuni mbali mbali kutojisahau sana na badala yake kuongeza umakini kwenye kipindi hiki ambapo tunategemea mashambulizi zaidi ya kimtandao kila mahali," Kileo alisisitiza.

Kwa mujibu wa ripoti liyotolewa na Orange Cyberdefence, imeaninisha ukuaji mkubwa wa uhalifu wa mtandao mwaka huu ambao kwa maelezo ya ripoti hiyo imeeleza uhalifu huu umechangiwa na matumizi makubwa ya mitandao yaliyo shuhudia kutokana na janga la UVIKO 19 ambapo huduma nyingi zilihamia mitandaoni.

Elimu, manunuzi ya bidhaa, afya na ufanyaji wa kazi ulitegemea zaidi mitandao na watu kubakia nyumbani iliyopelekea matukio mengi ya kihalifu mtandaoni kushuhudiwa.

Sababu nyingine ni wanafunzi wengi kubakia nyumbani na kutokana na uwezo wao mkubwa wa kujua mambo walionekana kuhusika kwenye matukio ya kihalifu mtandaoni.

Aidha, uhalifu unaolenga taarifa zinazopatikana kwenye simu zetu nao umeendelea kukua.

Kumekua na wimbi kubwa la programu tumishi zenye malengo mabaya wa kuiba taarifa za watu huku watumiaji wengi wakiwa hawana elimu ya kutosha ya namna ya kutambua, kujilinda na kujikwamua kwenye tatizo pale wanapojikuta kuwa wahanga wa matatizo ya kiuhalifu mtandaoni kwenye simu zao.

Watumiaji wa simu kujilinda

Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka wa AfICTA, Bw. Kileo alielezea mambo kadhaa yanayopelekea uhalifu wa mtandao kwenye simu zetu ambapo aliainisha changamoto kubwa ni watumiaji simu kuwa na tabia ya kupakua program tumishi mbali mbali bila kufahamu zina uwezo wa kuchukua taarifa zao.

Aidha, ulinzi dhaifu kwenye simu nao umeonekana kuwa changamoto kubwa, simu nyingi zimekosa nywila na yingine kuwa na nywila dhaifu huku programu tumishi maalumu za kusaidia ulinzi wa taarifa kwenye simu kutopatikana kwenye simu zetu.

"Watu wanasahau simu zetu zimekuwa zikitumika kwa kiasi kikubwa sana kwenye kufanya miamala na pia kuwa na muingiliano wa moja kwa moja na mifumo ya ofisi zetu ndio maana utakuta mtu anaweza tuma na kupokea barua pepe kupitia simu - Bahati mbaya simu hizi mbali na kuwa na taarifa zetu muhimu za miamala na za kiofisi tumeendelea kutokuwa na tabia ya kuziongezea ulinzi," Kileo alisisitiza.

Kwasasa bara la Afrika linakadiriwa kupoteza bilioni 4.12 za Marekani kutokana na uhalifu wa mtandao kwa mwaka huu wa 2021.

Changamoto kubwa ikiwa ni kukosekana kwa elimu ya uelewa, ushirikiano wenye malengo wa kukabiliana na uhalifu wa mtandao, vitendea kazi na upungufu mkubwa wa wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na uhalifu wa mtandao.(BBC)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news