Rais Dkt.Mwinyi ataja sababu za kampuni binafsi kupima UVIKO-19 uwanja wa ndege

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, sababu za kuipa kampuni moja zabuni ya kutoa huduma ya kupima Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ni kuongeza ufanisi na kuondoa kero ambazo walikuwa wanakumbana nazo watalii wanapofika nchini au wanapotaka kusafiri.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Desemba 11, 2021 katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar wakati akiwa katika mazungumzo na wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, kampuni hiyo binafsi ilipewa zabuni ya kutoa huduma za upimaji wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baada ya mchakato huo kuzingatia taratibu zote za manunuzi, kwa lengo la kuongeza ufanisi na ubora katika utoaji wa huduma hiyo.

Amesema, awali kabla ya zabuni hiyo kutolewa mgeni alilazimika kusubiri hadi siku nne ndipo apate majibu ya hali yake kuhusu UVIKO-19, lakini baada ya hatua hiyo kwa sasa ndani ya saa 24 majibu yanakuwa yanatoka na mgeni anaweza kufuatwa popote alipo kupatiwa huduma ya vipimo, kulingana na hitaji lake.
Mheshimiwa Rais amesema, tangu wafanye hivyo kila mgeni na watalii wanatoa sifa kwa kazi nzuri inayofanywa na kampuni hiyo ambayo hakuiweka wazi.

"Majibu yanatoka ndani ya saa 24 na hakuna mtalii aliyechelewa ndege yake kwa sababu ya kukosa majibu, kutoka siku nne za awali hadi saa 24 ni mafanikio makubwa mno,"amesema Rais Dkt.Mwinyi.

Pia amesema kuwa, awali wageni wengine walilazimika kuhairisha safari zao kwa sababu hawajapata majibu ya UVIKO-19.

"Na hauwezi kusafiri, tukaona tukiendelea namna hiyo tutapoteza watalii na wageni wengi, hivyo tutoe tenda (zabuni) kwa kampuni binafsi ili tuongeze ufanisi, na hakika ufanisi unaonekana kwa sasa,"amesema.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, kampuni hiyo ilipata nafasi kutokana na ubora wa kazi zao pamoja na viwango vidogo vya makato ambayo wanachukua kwa kila gharama ya kipimo kinachofanyika kwa mgeni.

"Wengine walitaka kuchukua hadi dola 70 kati ya dola 80 zinazotozwa kwa ajili ya vipimo huku kinachosalia wakitaka Serikali ichukue, sasa tukaona hii ni changamoto, sasa kampuni hii wao walitaka kuchukua dola 30 tu kati ya dola 80 na hizo 50 zinaenda serikalini kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii, tukaona wanatufaa.

"Unaweza kujiuliza hiyo dola 30 wanachukua kwa ajili gani? Hiyo ni kwa ajili ya gharama za uendeshaji wa zoezi hilo na kufanyia matengenezo au kununulia vifaa wanavyotolea huduma,kwani vifaa vyote wanavyotumia ni vyao, hivyo hatua hii ni njema na tumezidi kupiga hatua,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.
Amesema, hatua hiyo imeongeza ufanisi mkubwa katika utoaji huduma kwa watalii uwanjani hapo, kwa kuwa uwanja huo ni eneo muhimu zaidi katika kutoa taswira halisi ya huduma za kitalii Zanzibar.

"Pia mazingira ya utoaji huduma katika uwanja wetu yameendelea kuwa na ufanisi zaidi, uwanja wa ndege ni sehemu muhimu sana katika Taifa, kwani hilo ndilo eneo ambalo mtalii au mgeni anapoanza kukanyaga kwanza, hivyo anapokutana na kero nyingi, zinapelekea usumbufu kwake, mtalii au mgeni huyo kumpata si rahisi tena, hali ndivyo ilivyokuwa kwenye uwanja wa ndege.

"Mtalii akifika anakutana na foleni kubwa ya kwenda kupata Visa, hiyo inamfikisha kwa Afisa Uhamiaji kwenda kulipa benki, akimaliza aende kwenye kipimo cha COVID-19 (UVIKO-19), akimaliza anasubiria mizigo. Mgeni anatumia muda mrefu kusubiria huduma sehemu hiyo hiyo, hii ilikuwa changamoto ndiyo maana tukaona kuna haja ya kufanya maboresho haya,"amesema.

Unataka kufahamu kwa nini Rais Dkt. Mwinyi anaweza kufanya mabadiliko muda wowote kuanzia mawaziri, wakurugenzi, wakuu wa mikoa na wilaya, endelea kusoma DIRAMAKINI BLOG taarifa zote utazipata kupitia blogu kutokana na mazungumzo na Mheshimiwa Rais.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news