RUWASA Pwani yaingia mikataba na wakandarasi 17

NA ROTARY HAULE

WAKALA wa Maji na USafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Pwani wametiliana saini ya mikataba na wakandarasi 17 wa ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya bilioni 7.8.

Hafla ya kutiliana saini hiyo imefanyika Mjini Kibaha huku ikishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge,Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Mwanasha Tumbo,Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi , Sekretarieti ya Mkoa pamoja na wadau wengine.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Beatrice Kasimbazi,amesema kuwa kwa awamu ya kwanza RUWASA wamepanga kutekeleza jumla ya miradi ya maji 17 yenye thamani zaidi ya bilioni 7.8.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Beatrice Kasimbazi (kushoto) akibadilishana mkataba na mkurugenzi wa fedha na Utawala kutoka kampuni ya ECIA Company Limited, Dotto Lwimo mara baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji katika hafla iliyofanyika Mjini Kibaha.

Kasimbazi, amesema kuwa miradi hiyo inatekelezwa katika Halmashauri zote zilizopo Mkoa wa Pwani kupitia mpango wa maendeleo wa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19,Mpango wa Malipo kwa Matokeo(PBR) na Fedha za Mfuko(NWF).

Amesema,kukamilika kwa miradi hiyo itawanufaisha jumla ya wakazi 45,071 ikiwa sawa na asilimia 3.9 ya wananchi waishio Vijijini hususani kwenye maeneo yenye mkusanyiko wa watu ikiwemo Taasisi za elimu na masokoni.

"RUWASA Mkoa wa Pwani tumejipanga kuhakikisha hadi kufikia Juni mwishoni mwaka 2022 miradi yote 17 iwe imekamilika na hii inatokana na muda mfupi uliowekwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo,"amesema Kasimbazi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa wakandarasi wanapewa dhamana kubwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya wananachi kwahiyo wahakikishe wanajenga miradi hiyo kwa kiwango kinachotakiwa.

Kunenge,amesema kuwa hatarajii kusikia miradi imechelewa kukamilika kutokana na visingizio vya wakandarasi kwakuwa kabla ya kusaini walijua kuna changamoto na tayari walijipanga kukabiliananazo.

"Mlivyokubali kusaini mikataba ya utekelezaji wa miradi yetu ya maji mlijua kuwa mtaweza kukamilisha kwa wakati kwahiyo sababu na visingizio vingine hatutazikubali maana tunahitaji maji kwasababu ya wananchi wetu na hata katika kusaidia wawekezaji wa viwanda," amesema Kunenge.

Kunenge,ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutawajengea heshima wakandarasi hao huku akisema wawe na imani na Serikali yao kwakuwa lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji.

"Nawaomba sana ninyi wakandarasi miradi hii ikafanyike vizuri maana itamsaidia mwenyekiti wetu wa Chama katika kutekeleza ilani pamoja na wabunge wa eneo husika kwahiyo ni bora kujenga miradi inayotoa maji kuliko kujenga miradi mibovu,"amesema Kunenge.
Meneja RUWASA Mkoa wa Pwani Mhandisi Beatrice Kasimbazi (kushoto)akimkabidhi mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji mkurugenzi wa kampuni ya Federick Construction Company Limited Fredrick Mlaki mara baada ya kusainiana mkataba huo leo Mjini Kibaha.

Kwa upande wake mkurugenzi wa fedha na Utawala kutoka kampuni ya ujenzi wa miradi ya maji ya ECIA Company Limited Dotto Lwimo, amesema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa.

Lwimo,amesema kuwa kampuni yake itafanyakazi kikamilifu na kumaliza kwa muda uliopangwa kadri ambavyo mkataba unaeleza huku akiitoa wasiwasi Serikali juu ya utekelezaji wa mradi aliohupata.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Frederick Construction Co Limited Fredrick Mlaki ,amempongeza Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuleta maendeleo nchini.

Mlaki,amesema kupatikana kwa kazi ya ujenzi wa mradi wa maji katika kampuni yake imetokana na juhudi za Rais kutafuta fedha sehemu mbalimbali na kwamba lazima aunge mkono juhudi hizo.

Hatahivyo, ameahidi kutekeleza kazi aliyopewa kwa wakati ili kuendelea kuipa nafasi Serikai katika kuwaamini wakandarasi wa ndani kama ambavyo Serikali ya awamu ya sita inavyofanya.

Post a Comment

0 Comments