Simba SC yakataa kuvaa logo ya mdhamini mwenza GSM michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara

NA GODFREY NNKO

SIMBA SC imekataa kuvaa logo ya mdhamini mwenza wa Ligi Kuu Tanzania Bara ya GSM.

Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez amesema, wameandika barua Bodi ya Ligi kuomba ufafanuzi baada ya kuambiwa kuanzia mchezo ujao wanapaswa kuvaa logo ya mdhamini mwenza wa Ligi Kuu kwa maana ya GSM.
Hayo yanajiri ikiwa kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu au timu ikikataa kuvaa logo ya mdhamini inapigwa faini ya Shilingi Milioni Tatu kwa mechi na wakiendelea kukaidi wanashushwa daraja.
Mkataba waliosaini GSM na TFF hivi karibuni masharti yaliyopo kutoka GSM ni kuwa, logo yao inapaswa kukaa upande wa kushoto wa jezi.

Aidha, tayari Simba SC walishapewa logo hizo na mamlaka za soka nchini wazitumie kuanzia mchezo unaofuata wa Derby ya Kariakoo.

Hali hiyo ya mvutano inajiri ikiwa Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC) imesema imepokea malalamiko kutoka kwa wadau wa mpira wakiisihi kuchunguza udhamini uliofanywa na Kampuni ya GSM kwa Ligi Kuu Tanzania Bara kama hautaathiri ushindani wa soka nchini.

Wadau hao waliwasilisha malalamiko yao kwa maandishi ndani ya tume hiyo Jumatatu ya Novemba 29, 2021 kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa FCC, William Erio wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Erio aliyazungumza hayo wakati akitangaza maadhimisho ya siku ya ushindani duniani ambayo yalifanyika Desemba 6,mwaka huu kwa upande wa Tanzania.

Mtendaji huyo amesema, kama tume itakuja na tamko maalumu juu ya suala hilo baada ya kujiridhisha.

Malalamiko hayo yalipokelewa ikiwa ni siku chache tangu kampuni ya GSM kusaini mkataba wa Sh2.1 bilioni na Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF).

Mkataba huo uliosainiwa Novemba 23, 2021 unaifanya kampuni hiyo kuwa mdhamini mwenza wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania inayoshika nafasi ya nane kwa ubora Afrika ambayo kwa sasa inadhaminiwa na NBC.

Pia hilo limefanyika ikiwa ni muda mchache tangu kampuni hiyo ambayo ni mdhamini wa Yanga SC kutangaza kuzidhamini timu za Pamba na Coastal Union ya jijini Tanga.

“Tulishaanza mchakato wakutaka kujua kama kitendo hicho hakitaathiri ushindani katika soka na majibu ya suala hili yatatolewa baada ya kujiridhisha kwa kuzingatia kanuni za ushindani na kama kweli linahusiana na ushindani,” alisema Erio.

Alisema katika barua waliyopokea miongoni mwa vitu vilivyohojiwa ni Je? Kwa kufanya hivi hakutaathiri ushindani na Yanga haitanufaika zaidi katika mashindano hayo kwa sababu mdhamini wao amedhamini na timu nyingine pia.

Yanga SC na Twiga mwekundu
Awali Yanga SC nao walikataa nembo nyekundu ya mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kupendekeza kutumia nembo nyeusi ya Benki ya NBC.

Baadae Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo alitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya vilabu vya soka nchini kubadili nembo za wadhamini kwenye jezi zao.

“Suala la nembo ni suala la kikanuni na bodi ya ligi kazi yake kusimamia kanuni mwenye dhamana ya kusimamia hilo ni yule mwenye nembo yake.

“Bodi ya ligi ina nembo yao, TFF ina nembo yao na kila klabu ina nembo yake. Bodi tutasimamia kanuni zinavyosema na pia tutazingatia makubaliano baina ya mwenye nembo na klabu husika.

“Na haiwezekani mwenye nembo aseme tumekubaliana na mhusika fulani halafu bodi ipinge, bodi ipo kwa ajili ya kusave interest ya klabu na bodi ya ligi ni sulihisho na si kuwa chanzo cha tatizo kwa wadau wetu,”Almasi Kasongo aliyabainisha hayo hivi karibuni wakati akitolea ufafanuzi kwa nini wamekubali Yanga SC kuvaa twiga mweusi katika jezi zao.

Post a Comment

0 Comments