Banda la Tanzania EXPO 2020 Dubai laendelea kuvutia wageni wengi

NA KASSIM NYAKI,UAE

BANDA la Tanzania katika Maonesho ya EXPO 2020 Dubai limeendelea kuvutia wageni wengi kutokana na uwepo wa maudhui ya picha na video za vivutio mbalimbali vya Utalii, madini ya thamani na vito mbalimbali ikiwepo Tanzanite, historia na utamaduni wa Tanzania, mazao ya kilimo, Miradi ya maendeleo, fursa za uwekezaji na ufundishaji wa maneno ya Kiswahili kwa wageni wanaotembelea banda hilo.
Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania ambaye pia ni Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu, Mhe. Mohammed Mtonga ameeleza kuwa uboreshaji (Branding) wa Banda la Tanzania katika maeneo ya kipekee na yenye mvuto ya Utalii, utajiri wa Madini, Miundombinu ya kimkakati, nishati, usafirishaji, utalii wa mambo kale na ufundishaji wa maneno ya lugha ya Kiswahili imekuwa chachu kwa wageni kuendelea kutembelea banda hilo.
Balozi Mtonga ameeleza kuwa tathimini ya utembeleaji wa Banda hilo kwa miezi mitatu ya mwanzo kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2021 imeonyesha kuwa zaidi ya wageni 92,629 wakiwemo viongozi kutoka nchi mbalimbali wametembelea banda la Tanzania.

“Hii inaonesha kuwa jitihada za Serikali ya Tanzania kupitia viongozi kuridhia na kusimamia maboresho ambayo sehemu kubwa maboresho yameshafanyika na imeongeza muitikio chanya kwa wageni kuja na wanapofika hapa wana vitu mbalimbali vya kuona katika banda letu ambavyo vina upekee na vyenye picha za uhalisia,’’amefafanua Balozi Mtonga.
Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika maonesho hayo Bi. Getrude Ngweshemi ameongeza kuwa sambamba na Tanzania kushiriki maonesho hayo pia imefanikiwa kutimiza lengo la kujenga mahusiano ya Kidiplomasia kwa nchi zaidi ya 50 zinazoshiriki maonesho hayo ambapo hili ni miongoni mwa mikakati wa Tanzania katika ushiriki kwenye maonesho hayo.
Ameongeza kuwa Tanzania inatumia vyema ushiriki katika jukwaa hilo ambapo tarehe 12 -17 Desemba, 2021 Tanzania kupitia Sekta ya Utalii ilikuwa na wiki ya utalii na tarehe 14 Desemba, 2021 lilifanyika Kongamano la Utalii lililokuwa la mafanikio. 

Aidha, tarehe 18 Desemba, 2021 Tanzania iliandaa Kongamano la kwanza la biashara na Uwekezaji ambalo lilivutia wadau mbalimbali na kuonesha kufanya biashara na Tanzania.

Kufuatia maonesho hayo wageni mbalimbali wameahidi kutembelea Tanzania baada ya Janga la Uviko 19 kwisha ambapo pia Wawekezaji kadhaa wameonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali.
Miongoni mwa taasisi za Tanzania zinazoshiriki maonyesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS).
Taasisi nyingine ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC) pamoja na Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Abu Dhabi na Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Dubai katika nchi ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu.

Maonesho hayo ya kimataifa yaliyoanza tarehe 1 Oktoba, 2021 yanaendelea hadi tarehe 31 Machi, 2022.
Wageni kutoka Mataifa mbalimbali wakiangalia picha za vivutio Vya Utalii vilivyopo Tanzania katika Maonesho ya EXPO 2020 Dubai, ambapo Tanzania ni Miongoni kwa Nchi 192 zinazoshiriki Maonesho hayo.
Lugha ya Kiswahili yaendelea kujulikana Kimataifa. Pichani Wageni mbalimbali Wakijifunza Maneno ya Kiswahili walipotembelea banda la Tanzania katika Maonesho ya Kimataifa ya EXPO 2020 Dubai ambapo Tanzania ni Miongoni kwa Nchi 192 zinazoshiriki Maonesho hayo makubwa Duniani. Maonesho hayo yaliyoanza Oktoba 1, 2021 yanaendelea hadi tarehe 31 Machi, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news