Mheshimiwa Othman ataja faida za vyama vingi vya siasa nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwepo kwa vyama vya siasa nchini ni jambo muhimu la kuongeza fikra bora zinazochangia kupatikana uongozi imara na serikali makini na hatimaye kuwaletea maendeleo wananchi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Januari 8,2022 katika Ofisi Kuu za Vuga jijini hapa, akiongea na waandishi wa habari na pia akitoa salamu zake kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo waliojitokeza kumpokea mara tu baada ya kuchukua Fomu ya Kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesisitiza kwamba siasa za vyama vingi siyo uadui bali ni njia muhimu ya kuelekea ujenzi wa serikali imara sambamba na ishara za uwepo wa demokrasia katika nchi.

“Serikali imara inatokana na fikra imara na pia vyama imara, na wala siyo jambo la kugombana na kuleta uadui,”amesema Mheshimiwa Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib.
Aidha, Mheshimiwa Othman amehimiza amani, umoja na mshikamano baina ya viongozi, wapenzi, wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo, wakati huu na baada ya Uchaguzi wa Ndani wa Chama hicho, kama ilivyokuwa kwa waasisi wake, akisisitiza kwamba kuna maisha baadaye.

Akisisitiza suala la umoja miongoni mwa wanachama, Mheshimiwa Othman amechukua fursa hiyo kuwaasa wagombea wengine juu ya siasa za kistaarabu zitakazoendeleza mshikamano, akisema lengo siyo kupigania kukimiliki Chama. 

Akikabidhi Fomu hiyo kwa Mheshimiwa Othman, Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya ACT-Wazalendo, Bw. Muhene Said Rashid amesema, lengo la zoezi hilo ni kuwapata viongozi watakaosimamia na kuendeleza mema yaliyotokana na Waasisi wa Chama hicho, akiwemo Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, na pia urithi wa kweli wa nafasi hizo ili kutekeleza matarajio ya wananchi ambayo ni pamoja na kuijenga na kuikuza Zanzibar.

Uchaguzi huo wa nafasi za Mwenyekiti wa Taifa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo upande wa Zanzibar, uliopangwa kufanyika kupitia Mkutano Mkuu Maalum wa Januari 29 Mwaka huu Jijini Dar es Salaam, unakuja kufuatia Kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea tarehe 17 Februari 2021, na pia kujiuzulu kwa mtangulizi wake ‘Babu’ Juma Duni Haji mwishoni mwa Mwaka 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news