Naibu Waziri Masanja azindua mafunzo kwa watoa huduma za utalii nchini

NA HAPPINESS SHAYO-WMU 

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amezindua rasmi Mafunzo kwa Watoa Huduma za Utalii nchini kuhusu Mwongozo wa Kukabiliana na janga la UVIKO-19 katika Sekta ya Utalii kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Kampasi ya Bustani jijini Dar es Salaam leo. Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Mary Masanja amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo watoa huduma za utalii namna ya kukabiliana na UVIKO 19.  

“Mafunzo haya yatawajengea uwezo watoa huduma za utalii nchini juu ya namna bora ya kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa kuzingatia matakwa ya kiafya na usalama pamoja na kuboresha huduma wanazotoa na hatimaye kimarisha ushindani wa nchi katika masoko mbalimbali ikiwemo kuvutia watalii wa kimataifa kuja nchini hasa katika kipindi hiki cha mtazamo mpya wa utoaji huduma za utalii na usafiri kukabiliana na UVIKO-19 yaani the new normal of tourism and travel,” amesisitiza Mhe. Masanja. Amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzindua Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, ambao utekelezaji wake umewezesha kufanyika kwa mafunzo hayo. 

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwafikia takriban watoa huduma 3,900 katika sekta ya utalii katika mikoa 26 nchini Tanzania. Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Philip Chitaunga amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika kuendelea kujengea imani watalii na ulimwengu kwa ujumla kuwa Tanzania imedhamiria kupambana na janga la UVIKO 19. 

Pia, amesema mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Watanzania wanaofanya kazi katika Sekta ya Utalii wanakuwa salama. Mafunzo hayo yatahusisha watoa huduma mbalimbali katika tasnia ya ukarimu na huduma za malazi na chakula kama vile katika hoteli, loji na kambi za kitalii; aina mbalimbali za waongoza watalii; watoa huduma katika shughuli za utalii wa kupanda mlima, uwindaji wa kitalii na utalii wa utamaduni; wakala wa safari za kitalii; wakala wa usafiri wa anga; na wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika na kutoa huduma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news