Aluminium Trailers Ltd kilichopo Kibaha ni kiwanda cha kwanza Afrika Mashariki kutengeneza matenki ya kusafirisha mafuta

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KIWANDA cha Aluminium Trailers Ltd chini ya Kampuni ya Lake Group kilichopo eneo la Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani ndicho kiwanda cha kwanza Afrika Mashariki kutengeneza matenki yanayosafirisha mafuta kwa kutumia magari.
Aidha, kina uwezo wa kutengeneza tenki moja kwa muda wa siku mbili kuanzia hatua ya mwanzo hadi kukamilika tenki lote ambapo hutumia malighafi ya Aluminium.

Akizungumza wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, Ofisa mwajiri na rasilimali watu wa kiwanda hicho, Hussein Ally amesema kuwa, kwa mwezi wanazalisha matenki 15 na wametoa ajira kwa watu zaidi ya 90.

Ally amesema kuwa, hadi sasa kiwanda hicho kimeshazalisha matenki 95 na mbali ya kuuza hapa nchini pia wanauza nje ya nchi.

Ally amesema, changamoto inayokikabili kiwanda hicho ni upungufu wa umeme na kuomba serikali iwezeshe kupatikana umeme wa uhakika ili kutokwamisha uzalishaji.

Kutokana na hali hiyo mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema changamoto hiyo inafanyiwa kazi ambapo tayari wamewasiliana na Waziri wa Nishati, January Makamba juu ya changamoto hiyo na pia Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuupatia kipaumbele mkoa huo juu ya miundombinu ikiwemo ya umeme kwani ni mkoa wa viwanda.

Alipotembelea kiwanda hicho na viwanda vingine vya uzalishaji mitungi ya gesi, matenki na mabomba ya maji, kiwanda cha chuma chuma, kiwanda cha uzalishaji gypsum na boti ambavyo vyote viko chini ya kampuni ya Lake Group, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea viwanda mkoani humo ili kujua mafanikio na changamoto zinazowakabili wawekezaji kwenye viwanda.

Kunenge amesema kuwa, umeme bado ni changamoto kwani umekuwa ukikatika mara kwa mara lakini mkoa utahakikisha changamoto hiyo inaondoka ili wawekezaji wasipate usumbufu wakati wa uzalishaji.

"Niliwaelekeza watu wa TANESCO kupitia viwanda vyote ndani ya mkoa ili kujua mahitaji yao ya umeme hasa wale wenye matumizi makubwa ili wapewe kipaumbele kwa kuwa na umeme wao na changamoto ya hapa itapatiwa ufumbuzi ili kazi zifanyike kwa ufanisi,"amesema Kunenge.

Aidha, amesema kuwa mkoa umetekeleza kwa vitendo sera ya viwanda ambapo mkoa huo una viwanda zaidi ya 1,438 huku vikubwa vikiwa ni zaidi ya 89 na vilivyobaki ni vya kati na vidogo.

"Uwepo wa viwanda vingi ni kuongeza pato kuanzia Taifa hadi kwa mtu mmoja mmoja kwani viwanda hivi vinalipia kodi na tozo mbalimbali lakini pia vinatoa ajira kwa wananchi hivyo lazima tuhakikushe tunaweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili kiwavutia na kupunguza changamoto," amesema Kunenge.

Viwanda vingine vya kampuni hiyo ya Lake Group alivyotembelea ni pamoja na vya uzalishaji mitungi ya gesi, matenki na mabomba ya maji, kiwanda cha chuma chuma, kiwanda cha uzalishaji gypsum na boti ambavyo vyote viko chini ya kampuni ya Lake Group, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea viwanda mkoani humo ili kujua mafanikio na changamoto zinazowakabili wawekezaji kwenye viwanda.

Post a Comment

0 Comments