RC Kunenge amtaka Mkandarasi daraja la Mbuchi kufanya kazi usiku na mchana

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Mbuchi lililopo katika Kata ya Mbuchi Tarafa ya Mbwera wilayani Kibiti, Alpha Logistics kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi hiyo kwa muda aliopangiwa.
Kunenge,ametoa maagizo hayo leo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo linalojengwa kwa usimamizi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kwa gharama ya bilioni 6.2.

Kunenge amesema kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo kwahiyo lazima likamilike kwa wakati sahihi.

Amesema,Mkoa wa Pwani unajivunia daraja hilo kwakuwa likikamilika litafungua fursa ya kiuchumi kwa Wananchi wa eneo hilo,Wilaya,Mkoa na Taifa ikiwa sambamba na kuondoa adha ya wananchi wanaovuka katika eneo hilo.
"Nichukue fursa hii kumpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kuboresha maisha ya Watanzania lakini Mkoa wetu unajivunia daraja hilo na hata lile la Wami kwakuwa kukamilika kwa madaraja haya ni mkombozi kwa wananchi wetu,"amesema Kunenge.

Kunenge ,ameongeza kuwa Rais ameamua kuifungua Tanzania na Mkoa wa Pwani ili kufika pasipofikika na imani yake kuwa eneo la Mbuchi litakuwa moja ya eneo litakalofikika kwa urahisi zaidi.

Amesema,eneo la Mbuchi ni nzuri kwa Uvuvi ,Kilimo na shughuli nyingine za Kiuchumi,kwahiyo ni vyema wawekezaji wakajitokeza kwakuwa kero ya barabara na daraja zinakwenda kumalizika hivi karibuni.

"Barabara na hili daraja zitakuwa zinapitika wakati wote,kwahiyo wawekezaji wanataka kuja kuwekeza huku Mbuchi waje haraka kwakuwa Serikali ipo kazini muda wote kwa ajili ya kuweka sawa miundombinu ,"amesema
"Kwa kazi kubwa anayoifanya mama Samia,naomba tumuombee ili aepukane na shari zote ili aweze kufanyakazi zaidi ya kuwatumikia Watanzania kwa kuwaletea maendeleo,"amesema

Kunenge,amesema Serikali imetumia uwezo wake kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa daraja hilo kupitia Tarura na kuongeza kuwa Tarura wanafanyakazi nzuri ambayo ndio matarajio ya Rais Samia.

Meneja wa Tarura Mkoa wa Pwani Mhandisi Leopold Runji, amesema kuwa daraja hilo lilianza kujengwa Januari 4 ,2021 mpaka Januari 3 ,2022 na kwamba muda uliotumika ni asilimia 100 ya muda wa mkataba ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 80.

Runji,amesema kutokana na mradi huo kushindwa kukamilika kwa wakati kwasababu mbalimbali Mhandisi mshauri aliishauri Tarura kumuongezea mkandarasi huyo wiki sita ili kumaliza kazi hiyo.

Amesema,daraja la Mbuchi linalounganisha na upande wa eneo la Mbwera linajengwa kwa urefu wa mita 61 na litamilika Januari 23 mwaka huu.

Diwani wa Kata ya Mbuchi Yusuf Mpili , ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia kwa kuwajali wananchi na kutatua kero hiyo kwa faida ya Wananchi wa eneo hilo.

Mpili,amesema kuwa wananchi wake walikuwa wanakabiliwa na adha ya kuliwa na Mamba huku wajawazito wakishindwa kuvuka kwenda katika kituo cha afya na hivyo kujifungua pembezoni mwa daraja hilo.
"Kwa kweli ninamshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kujenga daraja hili maana ni miaka mingi imepita wananchi wameteseka kwa kuvuka hapa,wengi wao wamepoteza maisha,watoto wamekufa,na wajawazito wamejifungulia hapa pembeni,"amesema

Mkazi wa Kijiji cha Mbuchi Muhidini Ally,amesema kuwa walikuwa wanatumia mitumbwi midogo kuvuka kwa gharama ya Sh.1000 na wakati mwingine wanapokosa fedha wanasimamisha shughuli zao za uzalishaji upande wa pili.

Hata hivyo,Ally amemshukuru Rais kwa upendo wake mkubwa wa kuwajengea daraja hilo na kusema kukamilika kwake kutawasaidia kuvuka kirahisi, kupunguza adha mbalimbali na kwamba hata shughuli za kiuchumi zitaongezeka kupitia daraja hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news