Waandishi washauriwa kutumia kalamu zao kufichua

NA LUCAS RAPHAEL

WAANDISHI wa habari mkoani Tabora wametakiwa kutumia kalamu zao kufichua miradi inayotekelezwa chini ya kiwango ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wahusika ikiwemo kufanyiwa marekebisho.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora, Ramadhan Kapela akizungumza katika mkutano maalumu wa kujadili bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, wengine kwenye picha aliyekaa katikati ni Mkurungezi wa Manispaa ya Tabora na aliyevaa suti ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tabora, Mohamed Katete.

Wito huo umetolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapela ambaye pia ni diwani wa kata ya Isevya katika mkutano maalumu wa kujadili bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema kuwa, wanahabari wanafanya kazi nzuri kutangaza yale yote yanayofanyika katika mkoa huo ikiwemo shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Aliwaomba kufuatilia miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za serikali katika manispaa hiyo na kufichua mapungufu watakayoyaona ili yaweze kufanyiwa kazi haraka iwezekenavyo ikiwemo kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.

Alisisitiza kuwa vyombo vya habari ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya jamii hivyo wataendelea kuwapa ushirikiano wa dhati ili kuwezesha jamii kujua nini kinachofanywa na halmashauri yao na serikali kwa ujumla. 

"Kalamu zenu zina nguvu, tusaidieni kufichua miradi yenye mapungufu na changamoto zozote zinazowakabili wananchi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kabla mambo hayajaharibika,"amesema. 

Mstahiki Meya alibainisha kuwa serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo wanahabari wanafursa ya kuandika habari nyingi ikiwemo ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo, barabara na miradi ya maji.

Aidha alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea fedha za kutosha ili kufanikisha utekelezaji miradi ya wananchi huku akibainisha kuwa watamwandikia barua ya kumshukuru.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tabora, Mohamed Katete alipongeza uongozi wa manispaa hiyo kuanzia Mstahiki Meya, Mkurugenzi Mtendaji (Dkt.Peter Nyanja) na Mkuu wa wilaya (Dkt. Yahaya Nawanda) kwa kusimamia vizuri na kwa uwazi miradi ya maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news