Waziri Mbarawa:Daraja la Tanzanite (Selander Bridge) kuanza kutumika wiki ijayo

NA MWANDISHI MAALUM-WUU

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameeleza kuwa magari yataruhusiwa kupita katika Daraja jipya la Selander (Tanzanite), kuanzia Februari Mosi, 2022 mara baada ya ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 100.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Balozi Aisha Amour, alipokagua Daraja jipya la Selander (Tanzanite), lililokamilika ujenzi wake kwa asilimia 100 na litaanza kutumika rasmi Februari Mosi, 2022, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Rogatius Mativila.

Ameongeza kuwa, daraja hilo litaruhusiwa kwa wananchi kulitumia bila malipo kwa saa 24 kwa siku.

Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.30 na barabara unganishi kilomita 5.2 lililogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 243
Muonekano wa Daraja jipya la Selander (Tanzanite) ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 na litaanza kutumika rasmi Februari 1, 2022, jijini Dar esa Salaam.

“Daraja hili ni muhimu sana kwa sababu litapunguza changamoto ya foleni, sababu daraja la zamani la Selander lilikuwa limeshazidiwa na wingi wa magari hivyo kukamilika kwake ni muarobaini kwa foleni za jiji la Dar es Salaam,”amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kutoa fedha za ujenzi na matengenezo ya miundombinu nchini ili Tanzania kufunguka zaidi katika miundombinu yake na hivyo kuchochea uchumi wa Taifa.

Aidha, Prof.Mbarawa amewataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha wanaweka alama zote muhimu za barabarani katika maeneo yote ili kuongoza vizuri watumiaji wa barabara na kupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika.

Vilevile amewaagiza Mameneja wote TANROADS nchini kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ili kuhakikisha inakuwa salama na kupitika wakati wote hasa hasa katika madaraja ili kuyakinga kutopata athari za mvua zinazoendelea kunyesha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mha. Balozi Aisha Amour, akitoa maelekezo wa uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), alipotembelea Daraja jipya la Selander (Tanzanite), jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Balozi Aisha Amour, amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha miundombinu ya barabara na madaraja inatunzwa na kusimamiwa kwa karibu ili kuzingatia thamani ya fedha.

Balozi Aisha, ametoa wito kwa wananchi wote wanaotumia miundombinu ya barabara kuhakikisha wanatumia kwa matumizi sahihi waliyoweka kwa kufata taratibu zote.

“Nitoe wito kwa wananchi na watumiaji vyombo vya moto kufuata matumizi sahihi ya alama na kwa madereva wapaki maeneo ya maegesho waliyowekea ili kusaidia kupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika,”amesisitiza Balozi Aisha.
Mhandisi wa Mradi wa Daraja jipya la Selander (Tanzanite), Mhandisi Manger Rajab, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati alipokagua daraja hilo lililokamika ujenzi wake kwa asilimia 100 na litaanza kutumika rasmi Februari 1, 2022 jijini Dar es Salaam.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS Mhandisi Rogatius Mativila, amemueleza Waziri huyo kuwa daraja mpaka sasa limekamilika kwa asilimia 100 na zoezi la kupitisha magari litaanza saa 12 asubuhi.

Mativila ametoa rai kwa watumiaji wa daraja hilo kuwa waangalifu na kuzingatia alama mbalimbali zilizowekwa ili kuepusha ajali.

Daraja jipa la Selander (Tanzanite) ni mojawapo ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka katika jiji la Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news