Yusuph Kileo awafungua macho Watanzania kuhusu uhalifu mtandao wa 'S.E attack'

NA GODFREY NNKO

MTAALAMU wa Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Digitali nchini, Bw. Yusuph Kileo ameshauri elimu zaidi iendelee kutolewa kwa Watanzania ili waweze kubaki salama dhidi ya mashambulizi ya wahalifu wanapotumia mitandao na kufanya miamala ya fedha.
Kileo ambaye ni miongoni mwa Watanzania waliobobea katika masuala ya usalama na uchunguzi wa makosa ya kidijitali ametoa rai hiyo leo Januari 9, 2022 wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG kuelezea namna ambavyo uhalifu wa mtandao aina ya Social Engineering (S.E) Attack unavyoanza kushika kasi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema, wahalifu wengi kwa sasa wanatumia uhalifu wa S.E attack hususani nchini Kenya kwa kuwasiliana na watu ambao huwaaminisha kuwa,wao ni wahudumu wa benki halisi, hivyo mwisho wa siku mhanga wa uhalifu huo anajikuta amewapatia taarifa zake zote, jambo ambalo ni hatari.

S.E attack ni aina ya uhalifu ambao umekuwa maarufu zaidi mtandaoni ambapo wahalifu huwa wanawateka wananchi au wateja wa benki kisaikolojia kwa kuwahadaa ili kutoa taarifa nyeti zinazowahusu. 

Kupitia aina hii ya uhalifu, mhalifu kwanza huchunguza mwathiriwa anayekusudiwa ili kuweza kukusanya taarifa muhimu zinazomuhusu, mashambulio ambayo kwa sasa nchini Kenya inatajwa kuwa, kati ya matukio 1000 ya kupigiwa simu,mpokeaji simu mmoja ujikuta akiwapa taarifa zote wahalifu hao na kujipatia fedha zake.

"Kikubwa zaidi, nashauri elimu zaidi indelee kutolewa kwa watu wetu hasa ukizingatia kuna changamoto za watu wengi kutoelewa namna ya kubaki salama watumiapo mitandao na kufanya miamala mtandao.

"Aidha, napongeza kampeni iliyofanywa, ingawa si kwa uzito sana ambayo ililenga makampuni ya simu pekee. Uhalifu mtandao unakuja na mbinu mpya na hili la mhanga (victim) kupokea simu kama imetoka kwa benki halisi au mtandao wa simu limeanza kushika tena kasi.

"Mara kadhaa nimekua nikisema uhalifu unaofanyika sehemu moja unaweza kufanyika sehemu nyingine pia, bahati mbaya ukisikiliza kwa makini mahojiano ya mhalifu na mhanga hususani audio niliyotumiwa kutoka nchini Kenya,kuna mambo kadhaa unaweza kuyagundua.
"Mosi, mhalifu ametumia aina maarufu ya uhalifu mtandao S.E attack. Mpokea simu ameona kama simu imetoka kwa benki halisi.Mpokeaji simu (mhanga) kutokana na kuchanganywa na maswali mengi amejikuta anatoa taarifa zake kadhaa huenda bila kujua athari zake.

"Mhalifu alipoombwa extension number alikata simu,nichukue nafasi hii kutoa wito kila mmoja kuhakikisha anaendelea kuchukua tahadhari dhidi ya uhalifu huu pamoja na mamlaka husika kuendelea kwa kushirikiana na taasisi za fedha kuendelea kutoa elimu kupitia mifumo mbalimbali ili kwa pamoja tuweze kuwashinda wahalifu wa mitandao ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakidhoofisha uchumi wa taasisi, watu na Taifa kwa ujumla,"amebainisha Kileo.

Post a Comment

0 Comments