BREAKING NEWS: Rais Samia awafuta kazi wakurugenzi kwa tuhuma za upigaji fedha za maendeleo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Buchosa, Iringa, Mbeya na Singida Mjini kwa matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maendeleo na upotevu wa mapato katika halmashauri hizo.

Ameyabainisha hayo leo Februari 4, 2022 akiwa njiani Magu jijini Mwanza akielekea Musoma mkoani Mara yanapofanyika maadhimisho ya miaka 45 tangu kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Siku ile tunazitangaza fedha nilisema kama mkurugenzi anataka kuona rangi yangu halisi achezee hizo fedha, sasa kwa taarifa zilizopo, Buchosa, Iringa, Mbeya na Singida Mjini, wakurugenzi wamechezea fedha. Mheshimiwa waziri (Waziri wa TAMISEMI) wakurugenzi hao nimewatengua sasa hivi” amesema Rais Samia nakuongeza,

“Yule wa Geita endeleeni na uchunguzi, na mimi timu yangu iko pale inafanya uchunguzi naye wakiniletea na makossa kama haya nay eye attatenguliwa,” amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Wakurugenzi hao ni kutoka Halmashauri ya Buchosa, Paul Malaga, Jiji la Mbeya, Amede Ng'wanidako,Manispaa ya Iringa, Bernard Limbe, Manispaa ya Singida, Zefrin Lubuva huku aliyekalia kuti kavu ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita Vijijini, John Wanga.

Aidha, amemuagiza Waziri OR-TAMISEMI, Innocent Bashungwa kuwasilisha ripoti za Wakurugenzi hao huku akiahidi kuendelea kumchunguza Mkurugenzi wa Geita Vijijini anayelalamikiwa na Mbunge wa jimbo hilo , Mheshimiwa Kasheku kukiuka utaratibu wa manunuzi kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa fedha za UVIKO-19.

"Baadae nitaomba nione ripoti yako inasemaje maana kuna kawaida ya kufichiana, lakini nina ripoti kabla ya kwenu,na hao Wakurugenzi nimewatengua sasa hivi,yule wa Geita Vijijini endeleeni na uchunguzi na Mimi timu yangu ipo pale inafanya uchunguzi naye akithibitika ana makosa kama haya atatenguliwa,".

Awali akitoa taarifa kwa Rais Waziri Bashungwa amesema wakurugenzi hao wamehusika na ubadirifu wa fedha ambapo kwa jiji la Mbeya walibaini kushuka kwa mapato na baada ya uchunguzi walibaini kuzimwa kwa mashine za POS 72 kwa zaidi ya siku 100 ili kuficha upotevu wa fedha.

Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Robert Gabriel amesema, walipokea fedha za kujenga vyumba vya madarasa pamoja na vyumba 32 vya shule shikizi ambapo kazi ilifanyika lakini kuna watu waliiba fedha.

Amesema, hawakupiga kelele baada ya jambo hilo hivyo kuna watu walikamatwa na wengine wapo ndani katika Halmashauri ya Buchosa lakini katika ujenzi wa vyumba vya madarasa fedha iliyobaki ni zaidi ya millioni 600.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news