Dkt.Serera: Tuendelee kumuunga mkono na kumuombea Rais Samia, mambo mazuri yanatekelezwa Simanjiro

NA MARY MARGWE

MKUU wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Dkt. Suleiman Serera amesema mipango ya Serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Simanjiro itatekelezwa kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma mbalimbali na hatimaye waendelee kuwa na imani na serikali inayowaongoza.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa na ziara ya kikazi ya kijiji kwa kijiji, ambapo alikuwa katika Kijiji cha Gunge, Ruvuremiti na Lerumo Kata ya Ruvuremiti yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wilayani humo.

Dkt.Serera amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma mbalimbali tena kwa wakati.

"Tuendelee kumuombea na kumuunga mkono kupitia juhudi zinazofanywa na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili aweze kutimiza ndoto zake kwa wananchi wa Simanjiro, ni mama mwenye maono na watanzania wake, katika kuhakikisha maendeleo ya wana Simanjiro yanatekelezwa kwa wakati na si vinginevyo,"amesema Dkt. Serera.

Aidha, amesema Serikali imejiandaa kikamilifu kutatua kero za papo kwa papo huku ikiweka mikakati mingi zaidi ili kutatua changamoto zote zinazowakabili wana Simanjiro kwa ujumla.

"Tumejadiliana kutatua kero za wana Simanjiro za papo kwa papo na kuweka mikakati ya wengi zaidi ili kutatua changamoto zote tulizozijadili," amrfafanua Dkt. Serera.

Dkt. Serera amefafanua kuwa, upatikanaji huduma ya maji, umeme wa uhakika, barabara zenye kupitika, uboreshaji wa huduma za afya, elimu, uwezeshwaji wa wananchi kiuchumi ni miongoni mwa mambo mengi yaliyotolewa mrejesho chanya, ambapo kwa Kata ya Ruvuremiti kazi hizo za upatikanaji za huduma hizo zinatekelezwa.

"Asanteni sana wananchi wa vijiji vya Gunge, Ruvuremiti na Lerumo kwa kujitokeza kwa wingi kuja kwenye mikutano mitatu kwenye vijiji vyenu, huu ndio uzalendo wa kweli ndugu zangu, kwani mnapokuja kwenye mikutano kama hii mnakuja kujua mambo mbalimbali yanayoendelea katika serikali yetu, lakini pia kitendo cha kuja na kuulizwa swali na ukajibiwa kiufasaha utakua unatoka hapa ukiwa na furaha na amani, hivyo endeleeni kuiunga mkono serikali chini ya uongozi wa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan," ameongeza Dkt.Serera.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news