Serikali yatoa taarifa njema kwa Watanzania waliopo Ukraine

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kuwa, hali za Watanzania waliopo nchini Ukraine ni nzuri na imechukua hatua za haraka kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 27, 2022 na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Buhohela.

Kupitia taarifa hiyo ameeleza kuwa,"Kutokana na hali ya usalama kuendelea kuzorota nchini Ukraine, Serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka ili Watanzania takribani 300 waliopo nchini humo kuondoka na kuingia katika nchi za Poland na Romania ambako kuna utulivu,"ameeleza kupitia taarifa hiyo.

Pia amefafanua kuwa, hatua hiyo inatoa fursa kuwawezesha raia wote wa Tanzania kurejea nchini kwa usalama.

"Aidha, Serikali inapenda kuujulisha umma wa Watanzania kuwa, mpaka sasa hakuna Mtanzania yeyote aliyepata madhara kutokana na hali inayoendelea nchini Ukraine.

"Tunawaomba wazazi wa wanafunzi, ndugu na jamaa wenye wapendwa wao nchini Ukraine, kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kuchukua hatua hizo,"ameongeza.

Wakati huo huo Serikali imesema itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu usalama wa hali za Watanzania hao kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.



Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news