Dkt.Nzunda:LITA mnapaswa kuwa chanzo cha elimu bora ya mifugo

*Pia awataka wakufunzi wa LITA kuwa chanzo cha kuandaa majarida mbalimbali vikiwemo vitabu vya ufugaji

 NA EDWARD KONDELA

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Bw. Tixon Nzunda ameitaka Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kuwa chanzo cha elimu bora ya mifugo ndani na nje ya nchi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na uongozi na wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA), na viongozi wengine kutoka wizarani, mara baada ya kufungua kikao cha tisa cha baraza hilo kilichofanyika jijini Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo).

Bw. Nzunda amesema hayo Machi 28,2022 jijini Dodoma wakati akifungua rasmi kikao cha tisa cha Baraza Kuu la Wafanyakazi la LITA na kubainisha kuwa ni wakati sasa wakala hiyo kuwa chanzo cha kuwashauri wafugaji na kutoa maarifa kwa wadau wa sekta ya mifugo ili sekta hiyo iweze kuimarika na kuwa ya kisasa zaidi.

Ameongeza kuwa wakufunzi wa LITA wanatakiwa pia kuwa chanzo cha kuandaa majarida mbalimbali vikiwemo vitabu vya ufugaji na kuwa chanzo cha kubuni na kupatikana kwa maarifa mapya yanayotokana na tafiti zinazofanywa na wakufunzi hao.

Aidha, katibu mkuu huyo amefafanua kuwa wajibu wa LITA ni kuwa karibu na umma kwa kutoa huduma bora ikiwemo ya wanafunzi wanaohitimu kuwa bora na wanaoheshimika, kutambulika, wenye maarifa, wanajiamini na kuandaliwa vizuri kwenda kusaidia sekta binafsi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Bw. Tixon Nzunda akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha tisa cha baraza hilo na kuitaka LITA kuwa chanzo cha elimu bora ya mifugo ndani na nje ya nchi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Awali Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la LITA Dkt. Pius Mwambene, akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa kikao hicho amesema wakala hiyo imeendelea kuimarisha mahusiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha inaboresha miundombinu ya kufundishia.

Dkt. Mwambene ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa LITA amefafanua kuwa kwa sasa wakala hiyo inakaribia kukamilisha makubaliano ya ujenzi wa kampasi ya LITA Mkoani Songwe ikiwa ni jitahada za kuongeza wigo wa elimu ya mifugo katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha wafugaji wanapata mwongozo wa ufugaji bora LITA imeanisha utaratibu wa kuwashikiza wanafunzi wa hatua ya nne kwa wafugaji katika maeneo yao wakati wa likizo ili kuanza kujenga uzoefu ujasiri wa kuwahudumia wafugaji mapema.

Pia, amebainisha kuhusu vikao vya Baraza Kuu la Wafanyakazi LITA, kuwa vinalenga kuishauri wakala kutekeleza majukumu yake kama ilivyoelekezwa kwenye sheria, kupokea na kujadili makadirio ya mapato kwenye matumizi ya wakala na kujadili mipango ya utekelezaji wake kwa ajili ya ustawi wa wakala na wafanyakazi wake.

Kufuatia malengo hayo amewataka wajumbe wa baraza kushiriki kikamilifu na kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya wakala.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi la Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha tisa cha baraza hilo kilichofanyika jijini Dodoma, na kubainisha kuwa wakala hiyo imeendelea kuimarisha mahusiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha inaboresha miundombinu ya kufundishia ukiwemo ujenzi wa Kampasi ya LITA Mkoani Songwe ambao uko katika hatua mbalimbali ili kuendelea kusogeza huduma kwa wananchi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Akitoa neno la shukrani baada ya kufunguliwa rasmi kwa kikao cha tisa cha Baraza Kuu la Wafanyakazi LITA, Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema wataendelea kusimamia maadili na weledi kwa wafanyakazi wa LITA na kuongeza ushirikishwaji ili kuwa na matokeo makubwa yenye maslahi mapana yatakayoleta tija.

Dkt. Mwilawa amefafanua kuwa nguvu zaidi zitaelekezwa kwenye maeneo ambayo yatagusa jamii na kwamba maelekezo yote yatafanyiwa kazi kwa kuweka vigezo na kupima vizuri ili kufikia malengo.

Amesema kuwa kila mfanyakazi aliyepo LITA atahakikisha anapata stahiki zake ili aweze kutekeleza majukumu yake kama anavyotegemewa katika kutoa mafunzo ya elimu bora ya mifugo kwa wanafunzi.
Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha tisa cha Baraza Kuu la Wafanyakazi la Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) jijini Dodoma, ambapo amesema wataendelea kusimamia maadili na weledi kwa wafanyakazi wa LITA na kuongeza ushirikishwaji ili kuwa na matokeo makubwa yenye maslahi mapana yatakayoleta tija. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Nao baadhi ya wajumbe wa baraza katika kikao hicho, wametoa maependekezo kadhaa ya kuboresha utendaji kazi pamoja na mazingira ya wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa morali na kufikia malengo ya LITA.

Wamesema kikao hicho ni muhimu katika kukumbushana utekelezaji wa mambo mbalimbali yakiwemo ya kiutawala kwa kuwashirikisha wafanyakazi na kutatua kero na kuwapatia taarifa sahihi kwa wakati ili kuondoa manung’uniko kazini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news