Rais Dkt.Mwinyi aonesha kutoridhishwa na hali ya usafi Zanzibar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza haja ya kupewa kipaumbele suala zima la usafi wa Mji wa Zanzibar kwani bado hajaridhika na hali ya usafi ilivyo hivi sasa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wadau wa Serikali za Mitaa Zanzibar, kulia kwa Rais ni Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said na kushoto kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ,Mhe. Masoud Ali Mohammed, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo Machi 7, 2022.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wadau wa Serikali za Mitaa kufuatia kikao cha madiwani pamoja na Mameya kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi kilichofanyika hivi karibuni Ikulu.

Amesisitiza haja ya kutumia kampuni zenye uwezo ama vikundi vya vijana ambao hatua hiyo itaweza kusaidia kutoa ajira pamoja na kupata usafi wa uhakika huku akisisitiza kwamba usafi wa mji lisiwe jambo la hiyari.

Pia amesema kuwa, yeye mwenyewe binafsi bado hajaridhika na usafi wa miji kwani miji haifanyiwi usafi unaotakiwa na wala taka hazikusanywi ipasavyo na Manispaa haijali.

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, licha ya hatua za makusudi zilizochukuliwa katika kuwekewa viluva pamoja na kupanda miti na majani katika barabara za mjini lakini bado hakuna ushughulikiaji wa kutosha na wala hakuna anayejali.

“Hili nalisema kwa mara ya mwisho na haiwezekani kulisema jambo hilo hilo kila siku...tafuteni njia mbadala wa kuweka usafi mji, njia mnazozifanya hivi sasa imeshafeli,”amesema Dkt.Mwinyi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameitaka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ pamoja na Mamlaka ya Mikoa kukaa na Manispaa zao na kujua muhusika wa ukusanyaji mapato katika maeneo husuka ya mji.

Amewataka wadau hao kukaa pamoja na kuorodhesha vyanzo vyote vya mapato sambamba na kujua jinsi ya ukusanyaji unavyofanyika.

Rais Dkt. Mwinyi alieleza azma ya Serikali ya kujenga miundombinu ya mji na kuitaka Manispaa kuchukua hatua za makusudi za kusimamia suala la usafi kwa wenye maeneo ya biashara yalioko pembezoni mwa barabara.

Katika maelezo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza haja kwa Manispaa kuwawekea maeneo maalum wajasiriamali ili kuepuka tabia ya kufanya biashara katika maeneo yasiyohusika.

Amewataka wadau hao kufanya michanganuo ya miradi mikubwa na Serikali iko tayari kuwachukulia dhamana ili miradi hiyo iweze kufanikiwa na kipato kiweze kupatikana. “Wakati umefika Manispaa isiwe omba omba...wala isitegemee pesa za leseni tu,”amesema.

Sambamba na hayo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwamba upo umuhimu wa kuzingatia kwamba watu wanahitaji kucheza hivyo, ni lazima viwanja vitengwe kwa ajili ya kucheza hasa ikizingatiwa kwamba hivi sasa viwanja vingi vinajengwa miradi ya maendeleo.

Alieleza kwamba maeneo yote ya wazi yatengenezwe vizuri na yawe maeneo ya michezo kwani michezo ina umuhimu wake na maendeleo yana umuhimu wake hivyo, ni vyema kila kiwanja kinachojengwa mradi basi ni vyema pakapatikana mbadala wake.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Mwinyi alieleza azma ya msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ya kujenga Ofisi za Mikoa yote mitano ya Zanzibar.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed amesema kuwa kwa upande wa mbadala wa Timu za Malindi na Mchangani ambazo katika eneo la viwanja vyao patakuwa na mradi tayari umeshapewa kazi Mfuko wa ZSSF kujenga viwanja vitatu vya kisasa ambavyo vitakuwa na taa pamoja na nyasi bandia katika eneo la viwanja vya Tumbaku.

Nao Wadau wa Serikali za Mitaa walieleza kufarajika kwao na maelekezo wanayopewa na Rais Dk. Mwinyi na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi hasa suala zima la usafi huku wakipongeza juhudi zake anazozichukua katika kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo endelevu.

Aidha, wadau hao walionesha azma ya kutaka kuwekeza miradi mikubwa ambayo itawapelekea kuweza kukusanya mapato zaidi na kuiomba Serikali kuwaunga mkono katika azma yao hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news