Rais Dkt.Mwinyi:Tutaendelea kumkumbuka Hayati Dkt.Magufuli kwa uongozi wake mahiri

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ataendelea kukumbukwa kutokana na uongozi wake mahiri.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo katika salamu za pole alizozituma kwa familia, ndugu jamaa, marafiki, wananchi pamoja na wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutimia mwaka mmoja tangu kutokea kifo cha Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa (CCM) Taifa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika salamu zake hizo za pole, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, anaungana na ndugu, jamaa na marafiki, wananchi pamoja na wanachama na viongozi wa CCM katika siku hii ya kumbukizi.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameendelea kusisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kumuenzi Hayati Magufuli kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dkt. Mwinyi katika salamu hizo pia, aliwasihi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waendelee kumuunga mkono na kumuombea dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aendelee kuongoza vyema ili nchi izidi kupata maendeleo endelevu.
Hayati Rais Dkt.Magufuli aliyezaliwa Oktoba 29, 1959 alifariki dunia Machi 17,2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar-es-Salaam ambako alikuwa akitibiwa.

Post a Comment

0 Comments