Rais Samia awaeleza ukweli viongozi wa Jeshi la Magereza,akemea chuki

*Asema ana taarifa kuna watumishi wanachungana kwa mabaya, kila mtu anamchunga mwenzake akosee iwe ishu

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema, wanaohukumiwa kufungwa jela wanaweza kupewa jina la wanafunzi kwa sababu shughuli kubwa ya Magereza ni pamoja na kujifunza na kurekebisha watu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Hamad Masauni na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Meja Jenerali Suleiman Mzee wakivuta kitambaa kuzindua Kiwanda cha Samani cha Magereza kilichopo Msalato jijini Dodoma leo Machi 25,2022.

Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Machi 25, 2022 katika uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwenye miradi ya makao makuu ya Magereza jijini Dodoma.

“Ni kweli kabisa ndugu zetu wanaohukumiwa kufungwa ni wafungwa, lakini tunaweza kuwapa jina la wanafunzi kwa sababu shughuli kubwa ya Magereza pamoja na adhabu ni kujifunza na kurekebisha watu kwa shughuli wanazojipanga nazo. Wakishirikishwa ipasavyo inakwenda kuwapa uzoefu na kwenda kuwapa taaluma, wakitoka waende kujitegemea haitaeleweka kama mfungwa anatoka hana la kufanya kama wale tulizoea kuwaona wakati wa msamaha.

“Mfungwa anasamehewa leo nje hana la kufanya hana pa kukaa familia inamkana. Anaamua kwenda tena kuiba kwa makusudi ama kwenda kufanya jambo ambalo ataonekana kufanya akamatwe arudishwe tena.

"Huo sio mwendo mzuri mwendo mzuri ni wanafunzi hawa wanapotoka kwenda kuweza kujitegemea kutokana na taaluma na ujuzi watakaokuwa wanapata wakiwa ndani,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Pia ameliagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha askari wake waliopanda vyeo kuendelea kutekeleza majukumu yao na kuacha tabia ya kurundikana ofisini pasipokuwa na kazi.

"Tulitoa ajira za askari 700 na wote wakapandishwa vyeo na mimi ndio mpandisha vyeo, haina maana mtu akipandishwa cheo asifanye kazi, warudi wakasimamie wafungwa, hatuwezi kuajiri kila mwaka, kama una cheo au hauna cheo na hauna kazi ya kufanya ofisini rudi field ukafanye kazi, cheo chako utabaki nacho wala hakiondoki hata kama unasimamia wafungwa.
"Msitulazimishe kuajiri watu wapya kwa sababu watu wengi wamepanda vyeo, mtanifanya sasa nisipandishe vyeo kwa sababu nikipandisha mnakuwa hamfanyi kazi, kwa hiyo hili la ajira sitatoa, nimezungumza siri na Kamishna Mkuu wa Magereza, sio siri tena ameniomba niajiri askari wengine ameniambia nipe tu hata wa darasa la saba niruhusu tu niajiri wakasimamie wafungwa.

"Kusimamia wafungwa kunataka uzoefu na mtu aliyefunzwa vizuri sasa ukiniambia nikupe tu hata darasa la saba, hata kama utawafunza kwa miezi mitatu, wale niliowapandisha vyeo ni wazoefu zaidi warudi wakasimamie wafungwa na sitotoa kwa sasa ajira mpya.

“Haina maana kama mtu ana cheo akabaki ofisini, hana kazi, na kama umepandishwa vyeo nina uhakika kuna watu wanazurura kwenye korido za maofisi hawana kazi, warudi wakasimamie wafungwa,"amefafanua Mheshimiwa Rais Samia.

Pia ameendelea kueleza kuwa, "Kuna tetesi nyingi nazipata ndani ya Jeshi la Magereza, nalisema hapa kwa sababu maofisa na maaskari wote mko hapa, inaelekea Jeshi la Magereza hamuongei lugha moja, wengine wanavuta Kusini wengine Kaskazini, nina taarifa kwamba mnachungana kwa mabaya kila mtu anamchunga mwenzie akosee iwe ishu, niwatake mdumishe umoja na mshikamano, mkiendelea kuvuta huku na huku hamtofika mbali.

"Jeshi hili sio mali yenu ni mali ya Watanzania, tumewaamini tu kuwapeni mtoe huduma kwenye jeshi, yoyote atakayekuwa tayari kurudisha nyuma kwa ajili ya nafsi yake nasi tutakwenda nae pamoja, mkishikana mtakwenda haraka zaidi, hampendani hamna umoja naomba rekebisheni, nendeni pamoja ili mfanye makubwa zaidi,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news