Rukwa warekodi mafanikio ya kipekee ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia madarakani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKOA wa Rukwa ndani ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imerekodi mafanikio ya kipekee.
Hayo yamesemwa Machi 18,2022 na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Joseph Joseph Mkirikiti wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia madarakani.

"Mkoa wa Rukwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajivunia uwepo wa amani na utulivu, umoja na mshikamano ambapo wananchi wa Mkoa huu wamekuwa wakiendelea kufanya shughuli zao za kujiongezea kipato bila vikwazo vyovyote.

"Katika Kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita (Machi 2021-Machi 2022), Mkoa umepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali za Elimu, Afya, Miundombinu ya Barabara, Maji na kadhalika,"amefafanua Mheshimiwa Mkirikiti.

Sekta ya Afya

RC huyo amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja mkoa wetu umepokea shilingi Bilioni 1.3 kwaajili ya ujenzi wa vituo vya afya vitano (05) fedha ambazo zinatokana na tozo ya miamala ya simu. Vituo hivi ni pamoja na Matanga, Kipeta, Chala, Mwazye na Kate.

"Aidha tumepokea Shilingi Bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya nyongeza katika hospitali za Wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga,"amesema.

Pia amesema kuwa, kwa upande wa Sekta ya Afya mkoa umefanikiwa kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Bilioni 1.4 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi Bilioni 2.5 mwaka 2021/2022 hatua iliyowezesha wananchi kuwa na uhakika wa matibabu katika vituo vya kutolea huduma.

Amesema, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Serikali ya Awamu ya Sita imetoa Shilingi Bilioni 1.04 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la damu salama.

Sekta ya Maji

Akizungumzia kwa upande wa Sekta ya Maji amesema, mkoa umepata mafanikio makubwa katika sekta hiyo ambapo jumla ya miradi 99 yenye thamani ya shilingi Bilioni 25.5 ilisainiwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji ambapo kati ya hizo shilingi Bilioni 16.6 zilipokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi hiyo ya maji na tayari miradi 39 imekamilika na inatoa maji.

Pia amesema kuwa, fedha zingine zinaendelea kupokelewa kulingana na asilimia ya utekelezaji wa miradi hiyo. Kukamilika kwa miradi hiyo 39 kumeongeza asilimia ya upatikanaji wa maji na kufikia asilimia 64 Vijijini huku mijini kukiwa na asilimia 86.

Sekta ya Elimu

Kwa upande wa Sekta ya Elimu katika kipindi cha mwaka mmoja, RC Mkirikiti amesema kuwa, wamepokea jumla ya shilingi Bilioni 16.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya elimu ya Msingi, Sekondari, Chuo cha Ualimu Sumbawanga na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Kati ya hizo amesema kuwa, Shilingi Bilioni 3.4 zimepokelewa kwa ajili ya Elimu bila Ada katika Shule zetu za Msingi na Sekondari, Shilingi Bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya sita za Sekondari za Kata, Shilingi Bilioni 8.6 kwaajili ya ujenzi na ukamilishaji wa Miundombinu ya shule kupitia Programu za EP4R, SWASH, GPE, LANES II, TCRP - 5441, TEA, TOZO na Serikali Kuu.

Aidha, shilingi Bilioni 3 zimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga kinachoendelea kujengwa katika eneo la Pito Manispaa ya Sumbawanga.

"Eneo lingine kwa upande wa elimu ambalo tunaona mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kutolewa kwa fedha shilingi Bilioni 2.035 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo cha VETA Sumbawanga ambapo ujenzi huo utakamilika mwezi Mei mwaka huu.

"Sambamba na hizo Serikali imetoa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima tawi la Rukwa.

"Mafanikio mengine ni idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika madarasa ya awali katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeongezeka kutoka wanafunzi 35,457 mwaka 2021 hadi wanafunzi 41,070 mwaka 2022.

"Kwa upande wa sekondari wanafunzi walioripoti Kidato cha Kwanza mwezi Januari, 2022 imeongezeka kutoka wanafunzi 16,540 mwaka 2021 hadi kufikia wanafunzi 17,053 mwaka 2022. Hii imetokana na mazingira mazuri ya ujenzi wa miundombinu yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita,"amesema.

Sekta ya Miundombinu ya Barabara

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa huo amesema, katika kuhakikisha kuwa barabara zinapitika kwa ajili ya kuinua uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Rukwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kujizatiti kuhakikisha kuwa barabara zilizopo chini ya TANROADS na TARURA zinatengenezwa na kupitika muda wote.

Barabara za TANROADS

"Ndugu wanahabari, katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkoa wetu umepangiwa Shilingi Bilioni 15 kwa ajili ya maendeleo na matengenezo ya Barabara ambapo hadi kufikia mwezi Machi tayari tumepokea jumla ya shilingi Bilioni 12.4 kwa ajili ya matengenezo na maendeleo ya barabara zilizo chini ya Wakala ya Barabara Tanzania.

Barabara za TARURA

"Kwa upande wa Barabara za TARURA katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita tumeshuhudia kuongezeka kwa bajeti ya wakala huo kutoka shilingi Bilioni 4.3 kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi Bilioni 12.3 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo ongezeko hili la fedha ni sawa na asilimia 186.

"Hili ni ongezeko kubwa sana ambalo halijawahi kutokea tangu kuundwa kwa Wakala huo wa Barabara na hasa ikizingatia kuwa Barabara za TARURA ndizo zinazowagusa wananchi hususan vijijini,"amefafanua RC Mkirikiti.

Sekta ya Kilimo na Mifugo

Amesema katika sekta hiyo mkoani Rukwa ni muhimu ambapo pia wamepata mafanikio mengi makubwa.

Kilimo

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita,RC Mkirikiti amesema soko la mahindi kupitia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) limeendelea kuimarishwa ambapo kwa mwaka 2021/2022 wakala wamenunua jumla ya tani 21,000 za mahindi ya wakulima zenye thamani ya shilingi Bilioni 10.8.

Aidha, uwepo wa soko hilo la NFRA limesaidia mahindi ya wakulima kupanda kutoka shilingi 25,000 kwa gunia la kilo Mia Moja hadi kufikia shilingi 65,000 hadi 70,000 kwa gunia la kilo mia moja mwaka huu.

"Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa wa kuwahakikishia wakulima wa Mkoa wa Rukwa soko la mahindi. Pamoja na Soko la NFRA bado soko la nje ya nchi la mazao yetu limekuwa ni la uhakika kutokana na mazingira mazuri ya biashara yaliyowekwa na Rais Samia,"amesema.

Mifugo

Amesema, kwa upande wa mifugo wamepokea jumla ya shilingi Milioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa majosho sita ya kuogeshea mifugo pamoja na dawa za ruzuku ya kuogeshea mifugo lita 961.5.

"Hii ikiwa ni jitihada ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha kuwa mifugo inakuwa na afya njema kwa ajili ya kuzalisha mazao yatakayouzwa ndani na nje ya Mkoa wetu wa Rukwa.

"Sambamba na hayo tumefanikiwa kuvisha hereni ng’ombe 225,055 kwa lengo la kuitambua mifugo tuliyonayo ili kupunguza wizi wa mifugo pamoja na uhamiaji holela wa mifugo kwenye mkoa wetu. Haya ni mafanikio makubwa kwa upande wa mifugo ambayo sisi kwenye mkoa tunajivunia,"amesema.

Nishati ya Umeme

Amesema, mkoa kupitia mradi wa REA Awamu Pili mzunguko wa tatu katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita wamefanikiwa kufikisha umeme katika vijiji 20 kwa thamani ya shilingi Bilioni 3.5 na kufanya vijiji vyenye umeme kwenye mkoa wetu kufikia 186 kati ya Vijiji 339.

Katika kuhakikisha Rukwa inakuwa na umeme wa uhakika Serikali ya Awamu ya Sita imetoa shilingi Bilioni 3.4 kwa ajili ya kujenga mashine umba mpya kubwa yenye uwezo wa 15 MVA katika kituo cha Kupoza Umeme Sumbawanga ambapo ujenzi huu unakamilika mwezi huu Machi hatua itakayofanya TANESCO kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme hadi kufikia 30 MVA. Kukamilika kwa mradi huu kutaondoa kabisa tatizo la umeme wa mgao.

"Mafanikio haya niliyoyataja ni muhtasari tu kati ya mafanikio mengi ambayo sisi Wanarukwa tumeyapata katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mwisho, niendelee kumshukuru tena Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutupatia fedha kwa ajili ya maendeleo ya wanarukwa. Pia nikishukuru sana Chama Cha Mapinduzi CCM kwa Ilani ya Uchaguzi inayogusa maisha ya wana Rukwa. Niendelee kumtakia Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita Afya njema katika kuwatumikia Watanzania na wananchi wa Mkoa wa Rukwa,"ameeleza RC Mkirikiti.

Post a Comment

0 Comments