Serikali yasisitiza umuhimu wa walimu wa maandalizi kupewa mafunzo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bw.Ali Khamis Juma amesema kuna umuhimu wa kupewa mafunzo walimu wa maandalizi ili waweze kutoa elimu bora kwa watoto.
Amesema elimu ya maandalizi ndio msingi ambao utamjenga mtoto kuwa raia mwema au kiongozi bora katika Taifa.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa maandalizi na msingi katika ukumbi wa Kituo cha Walimu Kitogani amesema, Elimu ya Zanzibar kwa watoto inaanzia maandalizi hivyo mafunzo hayo ni muhimu kwa walimu hao katika kujenga Taifa bora la baadae.Amesema, wizara itaendelea kufanya jitihada ili kuona malengo yanafikiwa.

Amesema, kuna tatizo kubwa hivi sasa kuona watoto wanafeli hawafanyi vizuri katika masomo yao, hivyo amesema ni imani yake kuwa Mafunzo hayo yatajenga msingi mzuri zaidi kwa watoto kwa kuona sasa wanakuwa nao karibu kwa kuwasikiliza na kuwasaidia ili waweze kujifunza kwani mtoto analomchukia mwalimu hata ufahamu wake unapotea.

Amewataka walimu hao kuongeza dhamira ya mafunzo hayo kwa kuboresha na kuongeza hamasa kwa watoto pamoja na kuwataka kuwaelimisha na wengine ili kunufaisha na wengine.

Amesema, kuna tatizo kwa baadhi ya Walimu wa Zanzibar kukosa uwajibikaji ipasavyo kwa kisingizio cha kuwepo msongamano wa wanafunzi madarasani, lakini pia zipo Skuli nyingine ambazo WanafunZi ni wangu lakini kutokana na kuwajibika ipasavyo zimekuwa zikipasisha vizuri.

Amewataka kujiongeza kwa kuongeza ubunifu kwa kuwa watafutaji ili watoto waweze kufanikiwa kwani Walimu ni wito na hawalipwi kama wanavyodhani bali huwa wanafidiwa tu muda wao.

Nae Mratibu wa Mafunzo hayo ambae pia ni Afisa Utumishi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bwana Hassan Hussein Hassan amesema katika Mafunzo hayo moduli zote zilizoelezwa ndio changamoto ambazo zipo ndani ya Skuli zao.

Amesema ni imani yake kuwa kila moduli iliyotolewa italeta mabadiliko chanya katika Skuli zao ikiwemo katika uongozi, Afya, michezo, kuandika mpango kazi na mengineyo.

Kwa upande wake Afisa Elimu Taaluma Msingi Wilaya ya Kusini mwalimu Mussa Manake Hassan amesema Wilaya ya Kusini umepiga hatua kwa kuongeza ufaulu wa Wanfunzi wa darasa la sita kutoka Wanafunzi 26 hadi 45 kwa mwaka huu pamoja na kidatu cha nne.

Amesema pia Wilaya umejipanga kuhakikisha ufaulu unaongezeka kwa kuanzia kuzifuatilia Skuli zote zilizopo ndani ya Mkoa huo, kuwajengea imani Walimu wao kwa kuwa na uzalendo pamoja na kupinga vitendo vya udhalilishaji.

Pamoja na mafanikio hayo wanatatizo la kuwepo kwa uhamisho wa ovyo kwa Walimu walioajiriwa mwaka 2020 kwa madai ya kuwa ni wagonjwa hali ambayo inawarudisha nyuma katika kutoa Elimu.

Kwa upande wao Walimu waliopatiwa Mafunzo hayo wameipongeza na kuishukuru Wizara ya Elimu na kusema kuwa Mafunzo hayo yamekuwa ni muangaza kwao kwani walishasahauliwa Walimu wa maandalizi katika kupewa taaluma hiyo.

Mafunzo hayo ya siku 10 yamewashirikisha Walimu wakuu wa Skuli za maandalizi na msingi kwa Wilaya ya Kusini Unguja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news